Wabunge wacharuka kupanda bei za mafuta

Muktasari:

Wabunge wa Tanzania waishauri Serikali kuweka ruzuku na kuondoa tozo katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini ili kukabiliana na kupanda kwa haraka ya bei za mafuta nchini.

Dodoma. Wabunge wa Tanzania wameishauri Serikali kuweka ruzuku na kuondoa tozo katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini ili kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta nchini.

Wameyasema hayo bungeni leo Alhamis Mei 5, 2022 wakati wakichangia hoja ya kupanda kwa haraka kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa iliyotolewa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Omary Kigua.

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma ametaka Serikali kuingia gharama kuagiza yenyewe mafuta, angalau ikakubali kuingia hasara kidogo.

Wabunge wacharuka kupanda bei za mafuta

“Hii hali si nzuri na bado mwezi ujao yatapanda tena kwa karibu Sh3, 800, hili suala halikubaliki lazima tuone namna ya kuondoa kodi tulizoziweka katika mafuta angalau kwa miezi mitatu ili mafuta yaweze kushuka,”amesema.

Simon Songe (Busega-CCM) amesema kuwa sasa hivi gharama za kusafirisha saruji kutoka Tanga kwenda Mwanza ni Sh130,000 hadi Sh160,000 jambo ambalo litaongeza bei ya mfuko wa saruji kwa Sh1,500.

“Nashauri Serikali kutafuta fedha za dharura kupeleka ruzuku kwenda kwenye mafuta walau tuweze kupunguza gharama za mafuta,’amesema.

Ameshauri pia kuondoa tozo walizoweka katika mafuta angalau kwa Sh400 hadi Sh500 kwa miezi mitatu ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo.

Dk Joseph Mhagama (Madaba-CCM) amesema kati ya Januari hadi sasa mafuta ya petroli nchini yamepanda kwa asilimia 92 na kwamba huo ni mzigo mkubwa sana kwa Watanzania.

Amesema hivyo gharama ya maisha kati ya mwaka jana na mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 92.

Ameshauri Serikali kuondoa tozo katika mafuta ambazo zinatumika katika gharama za uendeshaji wa taasisi za Serikali ili kutoa unafuu kwa wananchi.

“Zile ambazo hazina madhara ya moja kwa moja katika miradi ya maendeleo tushughulike na expenditure (matumizi) nyingine,”amesema.

Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni amesema ifike wakati kuacha kugeuza mafuta kama sehemu pekee ya kutafuta pesa na badala yake iondoe tozo.

Amesema anaona kuna shida katika manunuzi kwa bidhaa ya mafuta na hivyo kuitaka Serikali kuangalia hilo.

Festo Sanga (Makete-CCM) ameshauri Serikali kutafuta mkopo wa fedha kwa ajili ya kuweka ruzuku kwenye mafuta ili bei yake ipungue.

“Bei ya mafuta hadi yanafika Dar es Salaam 1,162 kwa lita lakini msalaba na mnyororo wa kodi na tozo zilizoko kwenye mafuta ni zaidi ya Sh1300 bei ya mafuta duniani ni ndogo kuliko mnyororo wa kodi na tozo,”amesema.

Ameshauri Serikali ione namna ya kupunguza tozo na kodi hizo.