Spika atoa maagizo kwa Serikali kupanda bei mafuta

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiiagiza Serikali kupeleka bungeni hatua za muda mfupi itakazochukua kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Muktasari:

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameiagiza Serikali kupeleka bungeni hatua za muda mfupi itakazochukua kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameiagiza Serikali kupeleka bungeni hatua za muda mfupi itakazochukua kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

 Dk Tulia ametoa maelekezo hayo leo Alhamisi Mei 5, 2022 mara baada ya wabunge kujadili hoja iliyopelekwa bungeni na Mbunge wa Kilindi (CCM), Omary Kigua.

Kigua alitaka Bunge liairishe shughuli zake na kujadili kupanda kwa bei ya mafuta kwa haraka nchini, jambo ambalo limezua taharuki.

Amesema kanuni ya Bunge ya 56 inatoa fursa kwa Waziri kupeleka kauli ya Serikali bungeni kuhusu jambo fulani.

Amesema kwasababu Bunge halikuazimia kuhusu jambo hilo, hivyo anamuuagiza Waziri wa Nishati, January Makamba kupeleka kauli ya Serikali bungeni Jumanne wiki ijayo.

“Kauli ya mambo hayo waliyoyajadili na hatua mbalimbali ambazo Serikali itazichukua kwenye jambo hili. Kwasababu ni jambo la dharura na lazima tulifanye kwa udharura,”amesema.

Amesema Bunge haliwezi kuahirishwa ili Serikali ikaandae majibu ya hoja hiyo kama mmoja wa mbunge alivyoshauri bali Waziri atapewa fursa Jumanne ya kupeleka kauli yake bungeni.

Amesema siku hiyo Waziri aeleze hatua za muda mfupi za kukabiliana na changamoto hiyo na kwamba kwa yale yanayohusu hatua za muda mrefu wataendelea kuipa muda Serikali wa kuendelea kujipanga.