Rais Samia amteua Jaji Teemba Mwenyekiti Baraza la Maadili

Muktasari:
- Jaji mstaafu Teemba anakuwa anakuwa Mwenyekiti wa tano wa Baraza la Maadili akitanguliwa na majaji wastaafu, Damian Lubuva, Hamis Msumi, Januari Msofe na Ibrahim Mipawa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua jaji mstaafu, Rose Teemba kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunusi inaeleza kwamba, uteuzi huo ni kuanzia Aprili 24 mwaka huu.
Jaji mstaafu Teemba anachukua nafasi ya Jaji mstaafu, Ibrahim Mipawa aliyemaliza muda wake, akiongoza baraza hilo tangu Agosti 16, 2019 alipoteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa awamu ya tano, John Magufuli.
Kwa mujibu wa kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 pamoja na marekebisho yake kinaeleza kuwa baraza litakuwa na watu watatu watakaoteuliwa na Rais, miongoni mwao akiwemo aliyeteuliwa kutoka miongoni mwa watu wenye wadhifa au wamewahi kuwa na wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu.
Aidha, Fungu hilo hilo la 26 kifungu kidogo cha (3) kinasema kuwa Rais, atateua mmojawapo wa Wajumbe wa Baraza kuwa Mwenyekiti.
Kazi kubwa ya Baraza la Maadili ni kufanya Uchunguzi wa Kina wa malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya viongozi wa umma waliotajwa katika Fungu la 4 la Sheria hiyo.
Aidha, uchunguzi huo hufuatiwa na uchunguzi wa awali ambao kwa mujibu wa kifungu cha 18 (2)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, hufanywa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.