Rais Samia anavyojenga haiba yake ya kisiasa, kifalsafa

Muktasari:

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, aliachiwa huru na wenzake watatu. Mbowe alikuwa akikabiliwa na kesi ya ugaidi. Muda mfupi baada ya kutoka korokoroni, Mbowe alikwenda Ikulu na akapokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, aliachiwa huru na wenzake watatu. Mbowe alikuwa akikabiliwa na kesi ya ugaidi. Muda mfupi baada ya kutoka korokoroni, Mbowe alikwenda Ikulu na akapokelewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kusanya maoni ya viongozi na wafuasi wengi wa Chadema, waliozungumzia mkutano wa Samia na Mbowe, jibu la jumla ni moja; Pongezi! Anapongezwa Rais Samia kwa kufungua ukurasa wa maridhiano. Anasifiwa Mbowe kwa kutokuwa na kinyongo.

Mbowe alipoachiwa huru, mchuano mkali ukawa baina ya Chadema na ACT-Wazalendo. Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe akitumia kofia yake ya uenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), alimwomba Rais Samia aingilie kati suala la mashitaka ya Mbowe.

Zitto alishambuliwa kwa kuonekana ‘kiherehere’, kwamba alimwombea msamaha Mbowe kwa Rais Samia bila kutumwa. Msimamo wa Chadema ulikuwa kutotaka Mbowe aombewe msamaha, bali aachiwe bila masharti kwa kuwa hakuna kosa alilotenda.

Weka kando hilo; Rais Samia alipokwenda Ubelgiji kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Ulaya (EU), alikutana na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu. Baada ya kikao hicho, Lissu alizungumzia hoja alizowasilisha kwa Rais Samia kuwa mojawapo ni kuingilia kesi ya Mbowe.

Chukua kilichowasilishwa na Zitto kwa Rais Samia, vilevile kilichosimuliwa na Lissu, utaona kwamba hoja ilikuwa moja isipokuwa lugha tofauti. Pengine na mazingira yenye kutofautiana. Zitto alizungumza kwenye mkutano wa vyama vya siasa na Rais Samia ndani ya ardhi ya Tanzania, Lissu yalikuwa mazungumzo ya wawili, Brussels, Ubelgiji.

Siku chache baada ya mkutano wa Samia na Lissu, kesi ya Mbowe iliingia sehemu ya uamuzi mdogo, ikiwa yeye na wenzake walikuwa na kesi ya kujibu au kinyume chake. Ikaamuliwa kwamba Mbowe na wenzake watatu walikuwa na kesi ya kujibu katika mashitaka matano kati ya sita waliyoshitakiwa nayo.

Lawama kwa Rais Samia zikawa nyingi. Matarajio yalikuwa baada ya mkutano wa Samia na Lissu, uamuzi wa mahakama ungekuwa kuwaondolea kesi ya kujibu Mbowe na wenzake. Halafu, viongozi wa dini nao wakaenda Ikulu kuzungumza na Rais Samia. Katika mazungumzo, wakamwomba tena Rais Samia alitazame suala la Mbowe.

Siku Mbowe na wenzake walipofikishwa mahakamani kuanza kujitetea, wakakutana na taarifa ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), kwamba hakuwa na nia ya kuendelea na kesi ya Mbowe na wenzake watatu. Shauri likaisha hapo. Kisha, Mbowe akaenda Ikulu kuteta masuala ya nchi na Samia.

Samia na Mbowe, mbele ya kamera na vipaza sauti vya wanahabari, walizungumza kwa tabasamu jinsi ambavyo wamekubaliana kushirikiana na kufanya siasa za kistaarabu kwa ajili ya nchi. Pongezi zimekuwa nyingi baada ya kauli hizo za Mbowe na Samia.


Muktadha ni nini?

Machi 9, 2018, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alifanya kitu ambacho kiliushangaza umma wa taifa hilo, lakini akaweza kufungua ukurasa mpya wa kisiasa. Alikutana na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga. Mkutano wao ulifanyika Ikulu ya Kenya, Nairobi.

Mkutano huo hakuna aliyeutarajia. Ulikuwa umepita miezi miwili tu tangu Kenya iweke historia mbaya. Uhuru alikula kiapo cha utumishi kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, kwenye Uwanja wa Kasarani, Nairobi. Hiyo ilikuwa Novemba 27, 2017. Halafu Raila naye akaapishwa na mwanasheria Miguna Miguna, halafu akajitangaza kuwa Rais wa Watu wa Kenya. Raila aliapishwa Uhuru Park.

Mtazamo wa kila mmoja ni kwamba nchi isingetawalika. Hali ya viapo vya viongozi hao ilisababishwa na mgogoro wa Uchaguzi wa Rais wa Kenya, Agosti 2017. Raila alipinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Uhuru. Mahakama Kuu Kenya ilitengua ushindi wa Uhuru. Uchaguzi wa marudio ukapangwa Oktoba 2017, Raila akasusa. Uhuru alishinda na kuapishwa. Raila naye aliapishwa.

Jambo moja ambalo Uhuru na Raila walifanikiwa kulidhihirisha kwa umma ni kwamba mlango wa maridhiano upo wazi wakati wowote kwa wenye nia ya mapatano, hata kama uhasama unaonekana ni mkubwa kiasi gani.

Kadhalika, Rais Samia na Mbowe wameonesha ni kwa kiasi gani mlango wa maridhiano ulikuwa wazi. Ni suala la utashi tu! Na siku zote ifahamike kuwa siasa zenye kuruhusu mashauriano na maridhiano ni bora mno kwa taifa. Chuki na visasi vya kisiasa hugawa nchi vipandevipande.


Falsafa ni ipi?

Kitabu cha Profesa wa Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Chuo Kikuu cha Southern California, Gerardo Munck, kinachoitwa “Modes of Transition and Democratization”, ndani yake kuna falsafa ambayo Samia anaitumia kuijenga haiba yake ya kisiasa. Na ndivyo Uhuru alifanya Kenya. Tena Samia anakwenda vizuri kuliko Uhuru.

Ndani ya kitabu hicho, Munck akishirikiana na mwanazuoni mwenzake, Carol Leff, katika kurasa za 356 na 357, wanaandika dhana ya Mapinduzi kutoka Juu (Revolution from Above), kama ilivyotokea Bulgaria. Ni dhana hii inayovifanya vyama vya upinzani nchini kupepesuka tangu mwaka 1992.