Rais Samia arejesha Sh100 zilizoondolewa kwenye mafuta

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amerudisha tozo ya Sh100 iliyokuwa ikitozwa katika mafuta ya petroli, dizeli nchini.


Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amerudisha tozo ya Sh100 iliyokuwa ikitozwa katika mafuta ya petroli, dizeli nchini.

Wizara ya Nishati iliondoa tozo hilo Februari 28, 2022 ikisema uamuzi huo umetokana na kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kunakosababishwa na vita kati ya Russian na Ukraine.

Leo Jumatano Machi 30, 2022 Rais Samia wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ametangaza kuirejesha tozo hiyo.

Amesema suala la upandaji wa bei za mafuta yamekuwa yakipanda tangu katikati ya mwaka jana na kwamba walichukua hatua yakupunguza tozo kwa mara ya kwanza ili kushusha bei ya mafuta kwa wananchi.

Hata hivyo, amesema mafuta yameendelea kupanda ambapo Waziri wa Nishati (Januari Makamba) akachukua hatua kipindi hicho cha kuondoa Sh100 ili ibakie senti 56.

“Lakini (Waziri) hakuangalia kwa upana zaidi. Kwamba hiyo ilikuwa tayari katika bajeti iliyopitishwa na Bunge kulikuwa na utata kidogo. Kwa hiyo tumekaa kama Serikali tumerekebisha kwa hiyo ile shilingi (Sh100) nimeagiza irudishwe,”amesema.

Amesema tathimini waliyoifanya imeonyesha hata kama shilingi (Sh100) wangeiondoa kwa mwenendo wa upandaji wa mafuta bado isingekuwa na athari (impact) ila wangejikosesha kile ambacho wanakusanya.

Amewataka wabunge, mawaziri wanaosimamia sekta hiyo kuwaambia ukweli wananchi kuwa vita ya Russia  na Ukraine imepandisha bei ya mafuta.

“Mafuta yanapopanda ndio kila kitu kinapanda nauli zitapanda, usafirishaji wa bidhaa utapanda. Sasa hivi kutoa kontena la bidhaa kutoka China kuleta Tanzania, kwa kontena nadhani la futi 40 lilokuwa dola (za Marekani) 1500 sasa hivi ni dola (za Marekani) 8,000 hadi 9,000,”amesema.

Amesema na hilo inaenda kuathiri bei za bidhaa na kuwataka viongozi kuwaeleza sababu za kupanda kwa bei ya bidhaa nchini.

Amewataka wawaambie wananchi ukweli ili wasikae kusema kuwa Serikali inakaa kimya na haichukui hatua.

Kuhusu mafuta ya kula, amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kuangalia upya uamuzi waliouweka kwa ajili ya kulinda viwanda vya nchini.

Amesema uamuzi huo ulilenga kulinda viwanda vya nchini lakini imeonekana badala ya kulinda, baadhi ya viwanda vimekufa na hivyo kusababisha bei ya mafuta ya kula kuwa juu.

“Sasa mmezuia mafuta ya nje hayaingii viwanda vya ndani havizalishi. Bila shaka wananchi watapiga kelele kwa sababu bei itakuwa kubwa,”amesema.