Rais Samia asihusishwe kuahirishwa maadhimisho ya CWT -Ndalichako

Muktasari:

  •  Waziri Ndalichako amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa walimu.

Dodoma. Serikali imesema Rais Samia Suluhu Hassan asihusishwe na kuahirishwa maadhimisho ya miaka 30 ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Angalizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu),  Profesa Joyce Ndalichako. Ndalichako amesema kuwa  taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii juu ya kuahirishwa kwa maadhimisho hayo hakuhusiani na Rais Samia.

“Maadhimisho yalikuwa yafanyike jijini Mwanza, Desemba 16, 2023. Rais aliridhia mwaliko wa CWT Novemba 14, 2023 kuwa mgeni rasmi, baadaye CWT waliomba kubadili tarehe ya maadhimisho na kutaka yafanyike Desemba 13,2023 badala ya tarehe aliyoridhia Rais,” imesema taarifa iliyotolewa na wizara hiyo.

Profesa Ndalichacho amesema Rais Samia alielekeza wataarifiwe tarehe waliyoibadili atakuwa na jukumu lingine, licha ya CWT kuendelea na maandalizi na kubadilisha hadi Desemba 16, 2023.

Waziri Ndalichako amewahakikishia walimu nchini kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wao.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyakazi wote wakiwamo walimu, ambao wanafanya kazi kubwa ya kuwalea na kuwajengea ujuzi watoto kwa ajili ya kujenga Taifa na ustawi kwa Watanzania.

Rais wa CWT, Leah Ulaya jana Desemba 12,2023 alitangaza kuahirishwa kwa maadhimisho hayo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Jumamosi, Desemba 16, 2023 kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ulaya akizungumza jijini Dodoma alitaja sababu ya kuahirishwa maadhimisho hayo ni  aliyekuwa mgeni rasmi Rais Samia kuwa na majukumu mengine.

Ulaya pia aliitaka kamati tendaji ya chama hicho kujadili na kupanga maadhimisho hayo yatafayika wapi na kwa utaratibu gani.