Rais Samia ataka mahusiano mazuri Wizara, Jeshi la Polisi
Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura pamoja na Makamanda wengine wa Jeshi hilo mara baada ya kufungua kikao kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye Shule ya Polisi Tanzania (TPS) mkoani Kilimanjaro. Picha na Ikulu
Muktasari:
- Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchini na Jeshi la Polisi kuwa na mahusiano mazuri.
Moshi. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchini na Jeshi la Polisi kuwa na mahusiano mazuri.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Agusti 30, 2022 wakati akifungua kikao kazi cha maofisa wakuu waandamizi wa makao makuu ya polisi na makamanda wa polisi wa mikoa na vikosi, kinachofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema Wizara na Jeshi la Polisi wanapaswa kurekebisha mahusiano yao na kuhakikisha wanakuwa karibu katika utendaji kazi.
"Kuna matumizi mabaya ya fedha zile zinazokuja za bajeti, lakini matumizi haya mabaya ya fedha yanaendana na uhusiano usioridhisha baina ya Wizara na Jeshi la Polisi"
"Kuna kesi kadhaa nazifuatilia, unakuta msingi wake kwa nini wizara na jeshi haviendi pamoja, msingi ni matumizi, Wizara inasema hivi, Jeshi la Polisi linasema vile, kanuni huku inafuatwa, kanuni huku inageuzwa" amesema mkuu huyo wa nchi na kuongeza
"Kwanza tuende tukarekebishe mahusiano ya Wizara na Jeshi la Polisi, lakini pili matumizi ya fedha. Kuna tabia ya viongozi wa jeshi kufanya mawasiliano moja kwa moja na ngazi za juu bila kupita wizarani, sasa hayo yawezekana tuliyatengeneza sisi viongozi lakini nataka yarekebishwe".
Amesema "Wizara na Jeshi la Polisi muwe karibu sana katika utendaji, nitakachokiuliza kwa IGP akinijibu, hicho hicho anijibu waziri nitakapomuuliza, kukiwa na jawabu tofauti ina maana wizara na jeshi hamko vizuri".