Rais Samia ateua, atengua, Makonda ndani
Muktasari:
- Leo Jumapili, Machi 31, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwapanga wasaidizi wake kwa kuteua,kutengua na kuhamisha.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uhamisho, uteuzi na utenguzi wa viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Makonda amehudumu nafasi hiyo takribani miezi mitano.
Aliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM, Oktoba 22, 2023 akichukua nafasi ya Sophia Mjema. Anaweza kuwa amehudumu muda mfupi zaidi kuliko watangulizi wake kwenye nafasi hiyo kama Nape Nnauye, Balozi Humphrey Polepole na Sophia Mjema.
Makonda amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam enzi za utawala wa awamu ya tano wa Rais John Magufuli.
Utenguzi wa leo Jumapili, Machi 30, 2024 umemkuta Profesa Joyce Ndalichako ambaye amewekwa nje ya baraza la mawaziri. Ni baada ya kuwa barazani kwa zaidi ya miaka nane.
Rais Magufuli alipotangaza baraza lake la kwanza la mawaziri Desemba 23, 2015 alimteua Ndalichako kuwa mbunge kisha akamteua kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Alikuwa miongoni mwa mawaziri wasiozidi watano ambao kwenye panga pangua za Magufuli kwenye miaka yake mitano hawakuhamishwa.
Hata hivyo, Rais Samia aliyeingia madarani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha Magufuli, kwenye panga pangua zake, alimhamishia Ndalichako kuwa Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Sasa Rais Samia ametengua uteuzi wake na Deogratius Ndejembi aliyekuwa Naibu Waziri wa Tamisemi amepandishwa na kuwa waziri akivaa viatu vya Ndalichako aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (Necta).
Oktoba 1, 2023 Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilimteua Fakii Lulandala kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM. Kabla ya hapo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Momba.
Takribani miezi mitano tangu akalie wadhifa huo, Rais Samia amemteua Lulandala kuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro.
Pia, Gilbert Kalima aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chana cha Mapinduzi (CCM) yeye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga.
Kwa maana hiyo, kwa sasa ndani ya CCM kuna nafasi za juu tatu zimebaki wazi ya Ukatibu Mkuu wa UVCCM, Katibu Mkuu Jumuiya ya Wazazi pamoja na ile aliyokuwa akiishikilia Makonda ya uenezi.
Yanaweza kuwa mabadiliko ya kimkakati kauelekea kuboresha ufanisi maeneo hayo kipindi ambacho nchi inaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu 2025.
Mkeka huo wa Rais Samia pia umemhamisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja kwenda kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais- (Muungano na Mazingira).
Pia umeshuhudia sura mpya ya Zainabu Katimba kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi akichukua nafasi ya Ndejembi.
Katika mkeka huo, Balozi Asha-Rose Migiro ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Mipango huku Dk Edwin Mhende akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Dk Mhende aliwahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Dart.
Rais Samia amemweka kando Amos Makalla aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Soma mkeka wote hapa chini-: