Rais Samia atoa msimamo mifuko ya vijana kuunganishwa
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika kongamano la kufunga mafunzo ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) lililoandaliwa na UVCCM na kufanyika Tunguu.
Muktasari:
- Hata hivyo, ameahidi jambo linaloweza kufanywa na Serikali ni kuongeza fedha katika mifuko hiyo ili kuwafikia vijana wengi zaidi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema pendekezo la kuunganisha mifuko yote ya uwezeshaji wa vijana kuwa chini ya wizara moja haliwezekani, akieleza kila sekta ina majukumu na mipango yake maalumu kwa vijana.
Hata hivyo, ameahidi jambo linaloweza kufanywa na Serikali ni kuongeza fedha katika mifuko hiyo ili kuwafikia vijana wengi zaidi na si kupunguza kama wanavyopendekeza baadhi ya wadau.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili Aprili 26, 2026, visiwani Zanzibar alipokuwa mgeni rasmi katika kongamano la kufunga mafunzo ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) lililoandaliwa na UVCCM na kufanyika Tunguu.
Kongamano hilo lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi lilikwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika Aprili 26, 1964.
Rais Samia ameeleza hilo wakati akijibu ombi la Mwenyekiti wa UVCCM, Mohamed Kawaida, aliyeishauri Serikali kuanzisha mfuko mmoja au kupunguza idadi ya mifuko iliyopo ili kurahisisha upatikanaji wa fedha kwa vijana.
Kawaida ameeleza wingi wa mifuko umesababisha mkanganyiko miongoni mwa vijana kuhusu sehemu ya kwenda kuzipata fedha na wakati mwingine inawapa ugumu wa kuwaelekeza vijana.
“Mwisho tunaomba; tunajua dhamira yako ya kuwainua vijana. Ndiyo maana ulianzisha mifuko mbalimbali ya kuwawezesha vijana. Hata hivyo, mifuko imekuwa mingi kiasi kwamba vijana wengi hatuna uelewa wa kutosha. Tunaomba uwe mfuko mmoja ili vijana wajue pa kupata fedha au ipunguzwe idadi yake ili iwe rahisi kueleweka,” ameomba Kawaida.
Alichokisema Kawaida ni kama kilichoshauriwa na wabunge wakati wakijadili Bajeti ya Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana na kuibua hoja ya utitiri wa mifuko inayowahusu vijana na kushauri iunganishwe ili yote isimamiwe na wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Joel Nanauka.
Katika kuendeleza mjadala huo, wabunge walielekeza hoja zao kwenye udhaifu wa muundo wa kifedha na utekelezaji wa programu za vijana, wakisema hali hiyo inapunguza ufanisi wa wizara.
Mbali na wabunge, wadau mbalimbali nao walishauri Wizara ya Vijana ambayo ni mpya inapaswa kuboreshwa kimfumo ili mambo yote yanayohusu vijana ikiwamo mikopo isimamiwe na wizara hiyo na si kuwa kama mratibu kwa kuwa, inawachanganya vijana.
Alichokisema Rais Samia
Katika hotuba yake, Rais Samia aligusia suala hilo akisema amelisikia pia huko bungeni na kwamba haiwezekani kuhamisha mifuko yote kwenda Wizara ya Vijana kwa kuwa, sekta mbalimbali kama kilimo, mifugo, uvuvi na madini zina programu zao za kuwawezesha vijana, ikiwamo ya Mpango wa Jenga kesho iliyobora (BBT).
Katika majibu yake, Rais Samia amesema haiwezekani kwa sababu kila sekta ina mambo ya vijana; mfano Wizara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bashiru Ally kuna mpango wa BBT na hiyo ni kwa ajili ya vijana.
“Kila sekta ina sehemu ya vijana na hapa nataka niliseme na lile nililolisikia kutoka bungeni na lile ambalo Kawaida amelizungumza kuunganisha mifuko yote kwenda wizara ya vijana hili haiwezekani,” amesema Rais Samia.
“Sasa tuchukue miradi hiyo tuipe Wizara ya Vijana, halafu Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo na yeye ana BBT inayohusu kilimo uchukue uipeleke vijana ina maana wizara ya vijana isimamie kilimo, uvuvi na tuna Madini na wenyewe wana BBT tuchukue fedha yake iende vijana hili haliwezekani,” amesema.
Amesema kila sekta itatekeleza ile miradi ya vijana iliyopo kwenye sekta yake na wajibu wa Wizara ya Vijana ni kuwasimamia sekta kuhakikisha wote wanatekeleza miradi ya vijana iliyowekwa kwenye sekta yake.
“Mwisho wa siku waziri wenu asimame aseme katika sekta ya kilimo vijana wamenufaika hivi, kulikuwa na miradi hii imetekelezwa hivi na vijana kadhaa wamenufaika na sekta ya uvuvi hivyo hivyo na zingine lakini kutaka zote ziende sekta ya vijana hili haliwezekani,” amesema Rais Samia.
Amesema jambo ambalo Serikali inaweza kufanya ni kuongeza kiwango cha fedha ili wanufaike vijana wengi zaidi huku akiahidi hivyo anaenda kutekeleza.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewahusia vijana kutafakari neno mshikamano.
“Nina fahari kusema kwa sasa nchi yetu ni salama yenye amani na utulivu, nimeacha neno mshikamano na hapa ndipo nataka vijana tutafakari neno mshikamano tunavyoenda hivi mshikamano wa Watanzania unaachia pole pole,”amesema.
Amesema amewaasa vijana wa chama hicho kutafakari neno mshikamano kwakuwa unaachia ngazi ya vijana, wamekuwa wakija na maneno tofauti ya kuwafanya wabaguane badala ya kushikamana.
“Hili nalikemea vijana wangu, niwaombe rudini kwenye mshikamano, msiharibu nchi yenu, kamataneni na shikamaneni. Mkishikamana adui hana nafasi ya kupita lakini mkikubali kutenganishwa, adui mnampa njia apite,”amesema.
Amesema ni muhimu vijana hao waungane kuwa kitu kimoja ili nchi ibaki salama kwa kupendana, huku akisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar si waserikali bali ni wa watu.
“Tulianza muungano wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar na baadaye Muungano wa Tanzania lakini baadaye vyama vyetu tukijua umoja ndiyo nguvu na tutafaulu vizuri,” amesema.
Awali, Rais Hussein Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwaasa vijana na Watanzania kulinda amani iliyopo na kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuchochea kuvunja amani iliyopo.
“Niwaase Watanzania wezangu hasa vijana kuona umuhimu wa kuendelea kuilinda amani na jujiepusha na vishawishi vinavyoweza kusababisha kuvunjika kwa amani yetu, Natambua UVCCM mna majukwaa mbalimbali ya kuwaelimisha vijana wetu, wito wangu endeleeni na kazi hiyo bila kuchoka,”amesema.