Rais Samia atuma salam za pole kufutia kifo cha Waziri Kwandikwa
Muktasari:
- Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salam za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo, kufuatia kifo cha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salam za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo, kufuatia kifo cha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa.
Kwandikwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ushetu Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, amefariki dunia usiku wa Jumatatu Agosti 2, 2021 akiwa hospitalini jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Jaffar Haniu imeeleza kuwa Rais amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho kutokana na mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma.
“Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa umma hautasahaulika, Kwandikwa alikuwa kiongozi shupavu ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu,”amesema Rais Samia.
Rais Samia amemtaka Jenerali Mabeyo kufikisha salam zake za pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na watu wote walioguswa na msiba huo.