Rais Samia awaachia vicheko wajasiriamali

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyabiashara wadogowadogo wa samaki alipotembelea Soko la Wamachinga Parking ili kujionea na kutatua changamoto mbalimbali katika muendelezo wa ziara yake mkoani Tabora leo Oktoba 18, 2023.

Dar/Tabora. Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Tabora imeacha tabasamu na matumaini kwa wajasiriamali wilayani Nzega, baada ya ahadi ya ujenzi wa soko la kisasa eneo la Nzega Parking linalotumiwa na wafanyabiashara wadogowadogo.

Jana, Rais Samia alitembelea eneo hilo na kueleza Serikali imetenga Sh4 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya na kutoa maelekezo kwa uongozi wa halmashauri kuhakikisha wajasiriamali waliopo wanapewa kipaumbele soko hilo litakapokamilika.

Pia, alitembea kwenye meza za wajasiriamali na kuzungumza nao akitaka kufahamu changamoto wanazopitia.

Bahati ya mtende ilimwangukia mmoja wa wajasiriamali hao, aliyekuwa akiuza bidhaa za gengeni kwa kuzungumza na Rais Samia ambaye alinunua bidhaa kutoka kwake.

Kama wafanyavyo wanawake wengine waendapo sokoni, Rais Samia alifika kwenye genge la mama huyo na kumuuliza hali ya biashara kisha bei ya nyanya na kununua mafungu yote ya nyanya yaliyopangwa mezani.

Pia, aliagiza afungiwe viungo vingine vya kupikia na kutoa ahadi ya kumpatia mama huyo Sh300,000 kuongezea mtaji wake.

Baada ya kutoka kwenye nyanya alikwenda eneo wanalouza samaki na kuulizia bei, huko alionyesha kushangazwa na bei juu ya kitoweo hicho na kumuuliza Mbunge wa Nzega mjini (CCM), Hussein Bashe:

“Mheshimiwa mbunge inakuwaje kama samaki huyu Sh1,000 maisha yanakuwaje hapa Tabora, maana hapo ni samaki, bado hujapata unga na viungo vya kumpika huyo samaki,” alihoji Rais Samia.

Wafanyabiashara hao hawakumuacha Rais Samia aondoke hivihivi, wakaeleza kilio chao cha mtaji, ombi hilo lilimfanya atoe maelekezo kwa katibu wake kurudi katika eneo hilo kukutana na wanawake hao wauza samaki.

Kituo kilichofuata ni katika kijiwe cha kahawa, alimkuta mwanamke mjasiriamali akiuza kahawa ambaye naye alielezea kilio chake cha mtaji na ugumu wa biashara.
Katika eneo hilo Rais Samia alikaa kwenye kiti kama ilivyo kwa wateja wengine, lakini hakunywa kahawa kwa kile alichoeleza alikuwa amefunga, huku nyuso za tabasamu zikitawala.

Alipouliza hali ya biashara mama muuza kahawa alijibu, “hali ni ngumu mama biashara nayo haiko vizuri, ukiuza Sh5,000 unairudisha kwenye matumizi, hivyo inaisha, kila siku natamani ningepata mtaji nifanye biashara nyingine hata ya magunia ya mpunga,” alisema mfanyabiashara huyo.

Ombi la mama huyu lilikuwa Sh500,000 ili aweze kununua magunia matano ya mpunga, Rais Samia akatoa maelekezo kwa msaidizi wake kumrudia mama huyo baadaye.

Atembelea skimu ya umwagiliaji

Awali, katika ziara hiyo Rais Samia alitembelea na kuweka jiwe la msingi kwenye shamba la mbegu la Kilimi, ambako kuna skimu ya umwagiliaji yenye ukubwa wa hekta 1,102.
Akitoa taarifa ya skimu hiyo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema eneo linalofaa kwa umwagiliaji ni hekta 860 na uzalishaji wa mbegu katika shamba hilo utafanyika kwa mwaka mzima.

Bashe alisema shamba hilo ni la kwanza la Serikali linalotumia teknolojia ya Pivot, ambayo ni ya kisasa kwenye kilimo cha umwagiliaji.

“Mahitaji yetu ya mbegu ni tani 120,000, mashamba yetu ya ndani yana uwezo wa kuzalisha tani 40,000, tukiingiza na nyingine kutoka nje ni tani 60,000. Ulitupa maelekezo kufikia mwaka 2025 tufikie asilimia 75 ya mahitaji na mwaka 2030 tuwe tumejitosheleza.

“Tunahitaji jumla ya hekta 300,000 ili kumaliza changamoto ya mbegu, kwa sasa tuna hekta 34,000, sawa na asilimia 10, tunaomba wakuu wa mikoa kama wana mashamba watupe nafasi,” alisema Bashe.

Akiwa katika eneo la Magiri, Halmashauri ya Uyui, Rais Samia alisimama na kuwasalimia wakazi wa eneo hilo na kueleza Serikali yake itatekeleza miradi yote ambayo ipo kwenye bajeti na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zao.

“Halafu kuna mambo mengine mnaweza msiyaone kwa urahisi, lakini yanafanyika, mfano Serikali inajenga shule kuanzia awali hadi sekondari hatuchangishi hata shilingi na tunaleta fedha za watoto kusoma, sasa usingekuwa mradi huu wazazi mngetoa fedha nyingi, ila badala yake Serikali imekuachia kipato ubaki nacho mfukoni,” alisema Rais Samia.

“Kwenye ruzuku ya mbolea tusingetoa rukuzu mfuko ungenunua Sh160,000 hadi Sh140,000, lakini tukasema hapana iuzwe Sh70,000, fedha nyingine zibaki mfukoni. Sasa mkisikia kupendwa ndiyo huku, kwa hiyo anayekupenda umpende.”

Akiwa katika Kijiji cha Puge, Jimbo la Nzega Vijijini, Rais Samia aliwataka wananchi kuchapa kazi, hasa katika eneo la kilimo na kupata mazao ya kutosha.

“Sasa hivi hakuna mazao ya biashara wala mazao ya chakula, yote ni biashara na chakula, kwa hiyo ukilima mpunga, mahindi, karanga au choroko ni mazao ya biashara. Serikali inajiandaa kuleta viwanda vidogo au vya kati katika maeneo yote kuyachakata yauzwe ndani na nje ya nchi,” alisema.