Rais Samia awaonya wateule wanaojikweza

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Halali Wilaya ya Wanging’ombe alipowasili mkoani Njombe kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi mkoani leo Jumatatu Agosti 8, 2022

Muktasari:

Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya wateule wake kuacha kujikweza na badala yake wahudumie wananchi kulingana na viapo vyao.

Njombe. Rais Samia Suluhu Hassan amewaonya wateule wake kuacha kujikweza na badala yake wahudumie wananchi kulingana na viapo vyao.

Mkuu huyo wa nchi amesema hayo leo Jumatatu Agosti, 2022 wakati aliposimama na kuwasalimu wananchi wa Kijiji cha Mayale kitongoji cha Halali kilichopo wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe.

Amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo kwa ajili ya kuhudumia wananchi hivyo mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na wakurugenzi siyo watawala.

"Huku juu hakuna watawala kwa hiyo mkuu wa mkoa siyo mtawala, mkuu wa wilaya hata mkurugenzi ni wahudumu wa kuhudumia watu na kama hawafanyi hivyo mtuambie haraka sana kwasababu tumekula kiapo kuhudumia watu" amesema Samia

Amesema kama kuna kiongozi hatekelezi hayo apewe taarifa ili achukue maamuzi kwakuwa wamekula kiapo ili kuwahudumia wananchi.

"Lengo ni Tanzania yote ipate maendeleo inanyanyuka watu wote wawe na furaha uchumi ukue na maisha yaendelee" amesema Samia.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia ameweza kutoa Sh15 bilioni katika Wilaya ya Wanging'ombe kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya elimu, maji, afya na ujenzi wa barabara.

"Kazi kubwa ndani ya mwaka mmoja umegusa maisha ya wananchi hawa na umeacha alama kubwa" amesema Mtaka.

Mbunge wa Wanging'ombe, Dk Festo Dugange amesema wilaya hiyo tangu kuanzishwa kwake haijawahi kuwa na miradi mingi ya maendeleo kama ilivyo sasa.

"Wakati wilaya hii inaanza haikuwa na hospitali ya wilaya wala kituo cha afya lakini ndani ya mwaka mmoja lakini ndani ya mwaka mmoja umetupatia zaidi ya 4 bilioni kujenga vituo vya afya" amesema Dk Dugange.