Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Samia awatoa hofu Watanzania chanjo ya Covid-19

Rais Samia awatoa hofu Watanzania chanjo ya Covid-19

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema asingekuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kuchanjwa chanjo ya Covid kama ingekuwa si salama.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema asingekuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kuchanjwa chanjo ya covid kama ingekuwa si salama.


Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano Julai 28, 2021  katika uzinduzi wa uchanjaji wa chanjo hiyo, hafla iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam.


Hatua hiyo inakuja baada ya wiki iliyopita Tanzania kupokea zaidi ya dozi milioni 1.05 za chanjo aina ya Johnson & Johnson zilizotolewa na Marekani kupitia mpango wa upatikanaji wa  chanjo Covax.


Katika mpango huo, wapo baadhi ya watu wanaopingana na harakati hizo wakieleza chanjo hizo sio salama na wapo wanaounga mkono, lakini kiongozi huyo mkuu wa nchi amewaondoa hofu wananchi kuhusiana na hilo.


Rais Samia alisema yeye ni mama wa watoto wanne, ni bibi wa  wajukuu kadhaa wanaompenda sana na yeye kuwapenda, ni mke pia lakini mbali ya yote ni  Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi wa nchi hii.


“Nategemewa kama mama, kama bibi, kama Rais, kama Amiri Jeshi Mkuu, nisingejitoa mwenyewe nikajipeleka kwenye kifo, nikajipeleka kwenye hatari nikijua kwamba nina majukumu yote haya yananitegemea .


“Lakini nimetoka kuonyesha umma wanaonifuata nyuma nikijua kama Rais ni mchungaji na nina watu wengi nyuma nawachunga na wananitazama mimi hivyo nisingetoka kujihatarisha,”amesema Rais Samia.


Rais amebainisha kuwa amekubali kwa hiari yake kuchanja akijua kwamba ndani ya mwili wake ana chanjo kadhaa ambazo ameishi nazo kwa miaka 61 sasa kwani tangu amezaliwa kuna chanjo mbalimbali wamekuwa wakichanjwa, mbali na zingine wanazochanjwa njiani wakiwa wanasafiri ikiwemo ya homa ya manjano.


Hivyo kwake  haoni hatari iliyoko na baada ya wanasayansi kujirishisha hivyo yupo tayari kuchanja na kuwa kuwaomba Watanzania wapuuze  yote wanayoyasikia kuhusiana na chanjo hiyo.


“Kwa wale ambao koo zao hazijaguswa, hawajapata madhara ya maradhi haya wanaweza kusema wanavyotaka. Lakini nenda leo Moshi, nenda Arusha ,nenda  Kagera, hata Dar es Salaam uonane na zile koo ambazo zimeshaguswa na haya maradhi wana maneno ya kukuambia na kama wangeweza leo wote wangekuwa hapa kutaka kuchanja kuepukana na ile hasara walioipata.


Kwa hiyo niombe sana tusivunjane moyo  lakini tupeane moyo kupigana na janga hili ambalo limeteremka duniani.
Mwisho.