Rais Samia aweka jiwe la msingi ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa

Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, pamoja na kuzindua mpango wa ugawaji wa vifaa vya kazi kwa wavuvi hapa nchini.

Hafla hiyo imefanyika leo Septemba 19, 2023 huko Kilwa Masoko mkoani Lindi ambako Rais Samia anaendelea na ziara yake akitokea Mtwara alikofanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuzungumza na wananchi.

Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko utajumuisha ujenzi wa jengo la utawala, eneo la maandalizi ya samaki kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi, kituo cha umeme wa kuhudumia uendeshaji wa bandari na kituo cha maji safi kwa ajili ya kuhudumia bandari.

Pia, itakuwa na kituo cha kuzuia majanga ya moto, kituo cha kuzalisha naitrojeni, eneo la matunzo na matengenezo ya nyavu za uvuvi, matanki ya kuhifadhia mafuta, gati na karakana ya matengenezo ya meli.

Kukamilika kwa bandari ya uvuvi kutaifanya Tanzania kuwa na bandari ya kwanza ya uvuvi ambayo itakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwa kuongeza ajira, kuongeza upatikanaji wa samaki wa lishe, kuongeza mapato ya Serikali.

Akizungumzia mradi huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema wizara yake inatekeleza mradi wa kukopesha boti za uvuvi na vifaa vingine vya uvuvi kwa masharti nafuu ya riba.

“Jumla ya boti 160 zilizogharibu Sh11.5 bilioni, zitatolewa kwa wavuvi wakiwemo wakulima wa mwani katika Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu, vyama vya ushirika vya wavuvi, vikundi na kampuni za uvuvi,” amesema.

Amesema bandari hiyo inakwenda kuongeza ukuaji wa uchumi na wanakusudia sekta ya uvuvi ichangie kwenye pato la taifa kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2026. Amesema hiyo itawezekana kwa kuwavuta wawekezaji kuja kufunga gati huko Kilwa Masoko.

Ulega amesema gharama ya jumla ya Sh280 bilioni kwa ujenzi wa bandari hiyo, ni jambo linaloonyesha dhamira ya dhati ya Rais Samia ya kwenda kuinua sekta ya uvuvi nchini na kuhakikisha inakuwa na mchango kwa maendeleo ya taifa.

“Meli 10 zenye urefu wa mita 30 zitakuja kuweka nanga hapa, mitumbwi 200 itaweza kupaki hapo na vijana takribani 30,000 wataajiriwa katika bandari hiyo na wengi wao watatoka mikoa ya Lindi na Mtwara,” amesema Ulega.

Akizungumzia hatua ya Serikali kutoa vifaa hivyo, mkulima wa mwani, Shukrani Shamte amemshukuru kwa kuwapatia mkopo wa boti wenye gharama nafuu, boti hizo zitawasaidia kwenye kilimo cha mwani hasa kwenye kina cha maji mengi na pia kubebea zao hilo kuja pwani.

“Tunakuomba utuletee vifaa vingine, wakulima ni wengi, boti tulizoletewa ni chache, mahitaji ni makubwa,” amesema Shukrani wakati akizungumza na Rais Samia kwenye hafla hyo ya ugawaji wa vifaa vya kazi.