Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh11 trilioni kutekeleza mradi wa Kanda ya Kiuchumi Bagamoyo

Muktasari:

  • Utafiti uliofanywa na timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi kuhusu utekelezaji wa Kanda Maalumu ya Kiuchumi ya Bagamoyo, (SEZ) umebaini kuhitajika Sh11 trilioni kutekeleza mradi huo.

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na timu ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi kuhusu utekelezaji wa Kanda Maalumu ya Kiuchumi ya Bagamoyo, (SEZ) umebaini kuhitajika Sh11 trilioni kutekeleza mradi huo.

Utafiti huo kutoka chuo hicho unasema Serikali italazimika kutafuta Sh1.6 trilioni ili kuweka miundombinu muhimu katika eneo hilo inayojumuisha barabara, maji na umeme.

Hayo yalibainishwa jana mjini Bagamoyo na timu ya wataalamu kutoka chuo hicho wakati wakitoa mada kwa Waziri mpya wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo.

“Kutokana na ripoti hii, angalau Sh11 trilioni zitawekezwa kutekeleza SEZ ya Bagamoyo,” alisema kiongozi wa timu hiyo, Dk Emmanuel Mchome.

Katika hafla hiyo, Profesa Mkumbo aliongoza timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Maeneo ya Uchakataji Mauzo ya Nje (EPZA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wengine kutoka wizara mbalimbali kupokea upembuzi yakinifu na ripoti ya kina ya mpango mkuu wa Bagamoyo SEZ.

Kufufuliwa kwa mradi wa SEZ wa Bagamoyo kumetokana na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuurejesha uhai baada ya kukaa kwa miaka kadhaa.

Rais Samia alisema hayo alipoongoza Mkutano wa 12 wa Wakuu Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC) Juni 25, 2021 ambao Tanzania ilikuwa kwenye mazungumzo na wawekezaji ili kufufua mradi huo.

Mradi wa Bagamoyo SEZ utajumuisha maeneo 19 yakiwamo eneo la viwanda, biashara na sehemu ya huduma huku zaidi ya viwanda 200 vikitarajiwa kuanzishwa katika kanda hiyo.

Kutakuwa na maeneo ya ujenzi wa viwanda na biashara huria pamoja na vifaa na bandari. Kanda hiyo itakuwa ya pili nchini baada ya kanda maalumu za kiuchumi ya Benjamin William Mkapa iliyoanzishwa mwaka 2006.

Hata hivyo, Profesa Mkumbo alisema kutokana na uamuzi wa Rais wa kutaka mradi huo uendelee, ni muhimu kwa Serikali kupata ripoti ya nini inahusu kuendeleza ili kuutekeleza.

Eneo la SEZ ya Bagamoyo lina hekta 9,800 huku hekta 5,473 zikiwa zimepimwa.

Kazi ya uthamini iliyofanyika hadi mwisho wa Juni, 2023, inaonyesha kuwa takriban wakazi 3,322, ambao wanamiliki hekta 2,422 watalazimika kupokea Sh75 bilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Charles Itembe alisema mradi huo ambao umejumuishwa katika mipango yote ya maendeleo ya Serikali ya miaka mitano tangu 2010, unatoa manufaa kwa Taifa katika ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alisema wananchi katika eneo la mradi walishiriki kwa karibu na wanatoa msaada kamili katika utekelezaji wake.