Rais Samia kutunukiwa shahada ya udaktari India

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akilakiwa na Watanzania mara baada ya kuwasili New Delhi nchini India kwa ajili ya kuanza rasmi ziara ya Kitaifa tarehe 08 Oktoba, 2023.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kutunukiwa shahada ya heshima ya udaktari nchini India, mbali na ile aliyotunukiwa nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na Taifa hilo la Bara la Asia.

Shahada hiyo ya heshima anayotarajiwa kutunukiwa Oktoba 10, mwaka huu ni ya pili kwake, tangu alipotunukiwa shahada kama hiyo kwa mara ya kwanza na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Novemba 30 mwaka jana.

Hata hivyo, wasomi wamesema ni heshima kwake na kitendo hicho kinaashiria kutambuliwa kwa mchango wa kiongozi huyo na kwamba hulka, weledi, werevu na umakini wake, unafanana na mtu mwenye shahada hiyo.

Taarifa kuhusu Rais Samia kutunukiwa shahada hiyo nchini India, imetolewa leo, Jumapili Oktoba 8, 2023 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba akiwa katika ziara ya mkuu huyo wa nchi, nchini India.

“Tumepata taarifa rasmi kuwa Chuo Kikuu kinachoheshimika hapa India cha Jawaharlal Nehru kimeamua kumtunukuia Mheshimiwa Rais wetu Shahada ya Udaktari ya Heshima,” amesema Makamba.

Katika taarifa yake hiyo, Makamba ametaja mchango wa Rais Samia katika kuimarisha mahusiano ya India na Tanzania na mafanikio katika diplomasia hasa ya uchumi ni miongoni mwa mambo yaliyochagiza chuo hicho kione haja ya kumtunuku shahada hiyo.

Mambo mengine kwa mujibu wa Makamba ni mafanikio katika kusukuma maendeleo yanayogusa watu moja kwa moja nchini, mafanikio katika utangamano wa kikanda, kuimarisha mahusiano ya kimataifa kwa ujumla na ushiriki wake katika umoja wa mataifa.

“Tunashukuru kwamba Rais anatambuliwa, anatambulika, anaheshimika na anaheshimiwa hata katika mataifa mengine kwa kazi kubwa anayoifanya na mchango mkubwa anaotoa katika mataifa kufanya kazi pamoja na kuwa na uhusiano mzuri,” alisema Makamba.


Nini maana yake

Akizungumzia hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu UDSM, anayeshughulikia taaluma, Bonaventure Rutimwa amesema kuna njia mbili za kupata shahada ya udaktari, ambazo ni kusomea fani husika na ile ya kupewa kwa heshima.

Kwa udaktari wa heshima, amesema hutolewa na chuo kwa kuzingatia kilichofanywa na mtunukiwa.

“Mafanikio ambayo mtu ameyaonyesha katika eneo fulani, ndiyo yanayozingatiwa zaidi katika kutoa shahada ya udaktari ya heshima,” amesema.

Hatua hiyo inayotarajiwa kwa Rais Samia, amesema inamaanisha chuo hicho kimetambua mchango wake katika kile anachokifanya kinafanana na mtu mwenye shahada hiyo.

“Hii maana yake chuo hicho kimetambua mchango wa Rais Samia ni mkubwa sana unaonyesha mtu mwenye hulka, umakini na weledi na welevu unaofanana na watu wenye shahada ya udaktari nchini humo,” amesema.

Majibu kama hayo, yametolewa pia na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Profesa Burton Mwamila aliyesema ni heshima na ishara ya kutambua mchango wake, ingawa sababu za kutunukiwa zitatolewa siku ya tukio.

“Kwa kawaida sababu za kutunukiwa au kilichokisukuma chuo hicho kimtunuku shahada hiyo kitaelezwa siku anapotunukiwa, maana ndiyo utaratibu, lakini ni heshima kubwa,” amesema.

Hata hivyo, amesema wakati mwingine maana ya shahada husika hutofautiana kulingana na sababu za kutolewa kwake, jambo ambalo litajulikana Oktoba 10.


Hii ndiyo Jawaharlal Nehru

Ni miongoni mwa vyuo vikuu maarufu nchini India na Duniani, chenye umri wa miaka 54, tangu kilipoanzishwa mwaka 1969.

Asili ya jina lake ni Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo, Jawaharlal Nehru.

Mbali na Rais Samia, Waziri Mkuu wa 37 wa Urusi, Dmitry Medvedev aliwahi kutunukiwa shahada kama hiyo na chuo hicho, mwaka 2012.