Rais Samia kuwafuta kazi DC, DED Mtwara
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
- Mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala za Mikoa yametamatika na uongozi wa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Vijijini, Hanafi Msabaha na Mkurugenzi wake, Tatu Issike
Dar es Salaam. Hatma ya mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wao, imeacha kilio kwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Vijijini, Hanafi Msabaha na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Tatu Issike.
Kilio hicho ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza leo atawafuta kazi, kwa kile alichoeleza utendaji wao umesababisha wananchi warudishe kadi za chama (Chama Cha Mapinduzi-CCM).
Rais Samia ametangaza dhamira hiyo mkoani Pwani leo, Jumapili Agosti 27, 2023 alipohutubia hafla ya kufunga mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, yaliyofanyika katika Taasisi ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani humo.
Katika hotuba yake hiyo, mkuu huyo wa nchi ameesema uwepo wa baadhi ya Wakuu wa Wilaya wanaohongwa fedha kuhamisha miradi na kuamua itekelezwe katika maeneo mengine.
“Mkuu wa Wilaya anahongwa, mradi anaacha kwenda unakotakiwa anapeleka usipotakiwa, kiasi kwamba wananchi wanafika kurudisha kadi za chama, sisi huku tuna haja kubwa mmetuacha fedha mmepeleka kule na kadi zenu hizo.
“Sina imani na Mkuu wa Wilaya anayesababisha kadi zirudishwe, Mtwara, Mkuu wa Wilaya yako sijui Hanafi (Msabaha) namtimua leo siwezi kustahimili kadi za chama zinarudishwa, nini Mkuu wa Wilaya yupo DED yupo yeye na DED wake,” amesema.
“Nini watu wana shida anaulizwa anasema unajua kule wengi wapinzani, so what si Watanzania wale? Kwani wao sio watu, tena wamejenga maana kigezo ilikuwa wajenge atakayefika mbali ndiyo mradi upelekwe kwake,” ameeleza.