Rais Samia kuzindua miradi ya Sh8.8 bilioni Tabora

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dk Batilda Burian akizungumzia ujio wa Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Tabora. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Akiwa katika ziara ya Mkoa wa Tabora kwenye Wilaya za Igunga na Nzega, atazindua miradi miwili yenye thamani ya zaidi ya Sh 8.8 bilioni

Tabora. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuzindua miradi miwili yenye thamani ya zaidi ya Sh 8.8 bilioni katika ziara yake ya siku mbili mkoani Tabora kuanzia Oktoba 17 hadi 18,2023.

Akizungumzia ziara hiyo leo Jumapili Oktoba 15, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dk Batilda Burian amesema Rais ataingia mkoani hapo jumanne na kulakiwa na wananchi na viongozi mjini Igunga.

"Tunatarajia kumpokea mpakani mwa Mkoa wa Tabora na Singida na baadae katika eneo la Chuo cha Veta kilichopo mjini Igunga," amesema

Chuo hicho kinaelezwa kukamilika kwa asilimia kubwa kikiwa kinahitaji kuwekewa mashine na vifaa vya ufundi.

Dk Burian amesema akiwa katika chuo cha Veta , Rais Samia Suluhu atazindua chuo hicho kilichogharimu Sh2.6 bilioni kikiwa kinatarajia kuanza kuchukua wanafunzi Januari 2024 na baadaye atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara Mjini Igunga kabla ya kuelekea Nzega.

Ameleeza kuwa akiwa Nzega atazindua shamba la mbegu bora linaloendeshwa kisasa lililogharimu Sh6.2 bilion ambalo linazalisha mbegu bora za kilimo na baadae kuzungumza na wananchi katika Uwanja wa Samora mjini Nzega.

Dk Burian amesema awali ilikuwa pia akazindue miradi katika Wilaya za Urambo na Kaliua lakini kutokana na ratiba kubana maeneo hayo hatakwenda na yatapangiwa muda mwingine.

Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Tabora inakuja baada ya kupita miezi 17 tangu alipofanya ziara yake Mei 2022 alipotembelea Wilaya za Uyui, Sikonge na Tabora.