Rais Samia kuzindua sera ya usimamizi wa Ugavi
Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Baraza la Eid El Fitr Kitaifa lililofanyika leo Machi 21, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Uzinduzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa Sera ya Taifa ya usimamizi wa mnyororo wa ugavi ya mwaka 2025, ambayo imegawa majukumu na ufuatiliaji katika manunuzi kwa taasisi za umma.
Shughuli hiyo itakayofanyika Aprili 8, 2026 jijini Dodoma, ina lengo la kuweka mkakati wa uwajibikaji na uwazi katika suala la manunuzi na kukuza uchumi, kuendana na Dira ya Taifa ya 2050 kwenye masuala ya ugavi.
Uzinduzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kupitia mnyororo wa ugavi.
Serikali inakuja na mpango huo unaolenga miaka 10 kutoa matokeo, huku ikiwa imetangaza mpango wa kubana matumizi katika mambo yasiyo ya lazima, hasa katika kipinci hiki cha mtikisiko wa kiuchumi kutokana na vita katika mataifa ya Mashariki ya Kati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Aprili 4, 2026, jijini Dodoma Kaimu Kamishna wa Idara ya sera za ununuzi wa umma wa Wizara ya Fedha, Alex Haraba amesema, sera hiyo imeandaliwa ili kuweka mfumo jumuishi na kimkakati wa kusimamia shughuli zote zinazohusiana na mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma, kuanzia upangaji, ununuzi, ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali, hadi usambazaji na uondoshaji mali za umma.
Haraba amesema sera hiyo inalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi zinapatikana kwa ubora unaotakiwa, kwa wakati na kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.
“Kwa muda mrefu shughuli za mnyororo wa ugavi zimekuwa zikitekelezwa kupitia sheria, kanuni na mifumo mbalimbali bila kuwa na mwongozo mmoja wa kisera, unaounganisha hatua zote, hali iliyochangia changamoto za uratibu,” amesema.
Amesema kutungwa kwa sera hiyo kunatarajiwa kuimarisha uratibu na usimamizi wa pamoja katika shughuli za ugavi, kuboresha matumizi ya rasilimali za umma na kuongeza ufanisi wa tija katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Kiongozi huyo amebainisha kuwa sera hiyo inaweka mkazo katika utawala bora, matumizi ya teknolojia, ushiriki wa sekta binafsi na makundi maalumu ya kijamii na kuhamasisha matumizi ya rasilimali na malighafi za ndani ili kukuza viwanda vya ndani na kuongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Maraba, kupitia utekelezaji wa sera hiyo, Serikali inatarajia kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kupunguza upotevu wa rasilimali, kuongeza ufanisi wa miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.