Rais Samia: Miaka 61 ya changamoto, mafanikio

Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

Wakati Tanzania ikiadhinisha miaka 61 ya Uhuru leo, Rais Samia amesema ilikuwa safari yenye changamoto na mafaniko mengi ambayo Taifa linajivunia.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za maadhimisho ya miaka 61 kwa Watanzania akisema safari ya kuifikia miaka 61 ya Uhuru imekuwa yenye changamoto na mafanikio mengi ambayo Taifa linajivunia.

Samia ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter leo Desemba 9, 2022 ikiwa ni kumbukizi ya siku ya Uhuru ulipatikana mwaka 1961.

Akiwatakia Watanzania kheri ya kuadhimisha kumbukizi hiyo, amewataka kutumia siku hii kutafakari na kuweka dhamira ya kuongeza juhudi na maarifa ya kulipeleka Taifa mbele na kwa kasi zaidi.

“Nawatakia kheri Watanzania wote katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru. Imekuwa safari yenye changamoto na mafanikio mengi ambayo Taifa letu linajivunia.

“Tutumie siku hii kutafakari na kuweka dhamira ya kuongeza juhudi na maarifa ya kulipeleka Taifa letu mbele na kwa kasi zaidi,” ameandika.

Wakati akitoa salamu hizo, mwaka huu Serikali imefuta sherehe za maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru na Sh960 milioni zilizotakiwa kutumika kwenye maadhimisho hayo zitakwenda kwenye ujenzi wa mabweni ya shule zenye uhitaji maalum.

Hayo yalielezwa Desemba 5, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Simbachawene alisema tayari Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi) imebainisha Mikoa itakayonufaika na fedha hizo ambayo ni Shinyanga, Singida, Tabora, Lindi, Manyara, Njombe, Arusha na Rukwa.

Simbachawene alisema mwaka huu maadhimisho yatafanyika katika ngazi ya wilaya kwa kufanya midahalo na makongamano ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya kijamii.

“Kwa muktadha huu Waziri Mkuu ameniagiza kushirikiana na Waziri wa Tamisemi kufanya usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya midahalo na makongamano hayo ili kujiridhisha na matokeo yake,” alisema Simbachawene.

Kabla ya makongamano hayo, ratiba za Wakuu wa Mikoa na Wilaya zitatanguliwa na shughuli za kijamii ikiwemo kufanya usafi katika maeneo ya huduma za kijamii kama Hospitali, Shule, nyumba za wazee na nyinginezo.