Rais Samia: Msilitumie kanisa kufanya mambo ya hovyo, kemeaneni
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT) Dk Dickson Chilongani wakati wa sherehe za ufunguzi wa jengo la kitega uchumi (Safina House) la Kanisa hilo lililopo katika viwanja vya Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Jijini Dodoma Agosti 15, 2023.
Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan amefungua jengo la kitega uchumi la Kanisa la Anglikana Tanzania huku akiwataka viongozi wa dini kuliweka Taifa katika mikono salama ya Mungu.
Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka waumini wa Kanisa la Anglikana Tanzania kukemeana pale baadhi ya watu wanapolitumia kanisa kufanya mambo ya hovyo.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 15, 2023 wakati akifungua jengo la kitega uchumi linalomilikiwa na Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), linalojulikana kama Safina House.
Rais Samia amehimiza kazi ya kulinda maadili, kukemea maovu na kuwafundisha vijana kuhusu maadili mema.
“Lakini mbali ya vijana hata wakubwa ambao wanalitumia kanisa kufanya mambo ya hovyo naomba kemeaneni,”amesema.
Pia, Rais Samia amewasihi viongozi wote wa dini nchini kuendelea kuliweka Taifa katika mikono salama ya Mungu ili lidumu katika amani, umoja na mshikamano na kamwe wasikubali kuyumbishwa na mtu yoyote asiyeitakia Tanzania mema.
Akijibu maombi ya kanisa hilo kuhusu kurejeshewa kiwanja kilichopo nyuma ya jengo la Mackay, Rais Samia amesema amelichukua ombi hilo na atakwenda kulifanyia kazi.
Awali Askofu wa DCT, Dk Dickson Chilongani alisema kuwa jengo hilo lilianza kujengwa tangu mwaka 2017, limejengwa kwa gharama ya Sh8 bilioni.
Amesema kati ya gharama hizo Sh2 bilioni ni msaada kutoka kwa marafiki zao wa nchini Marekani, Sh3 bilioni ni jitihada zao za ndani na Sh3 bilioni ni mkopo.
“Kwa kutumia mapato haya na jitihada zetu za ndani ni dhahiri kwamba mkopo huo tutaulipa kipindi kifupi…Kila kanisa lilitoa mchango kwa kununua hisa na sehemu ya faida itakayopatikana kwa kupandisha jengo hili itatumika katika kusaidia kuwatunza wachungaji na wahudumu wengine,”amesema.