Rais Samia: Najiamini kufungua uwanja wa siasa

Muktasari:

  • Machi 19, 2021, Samia Suluhu Hassan, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania akichukua nafasi ya John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kujiamini kwake ndiko kunakomfanya afungue uwanja wa siasa kupitia maridhiano na kwamba atatekeleza makubaliano yote bila kupiga chenga.

Kauli hiyo ya Rais Samia inakuja wakati anakabiliwa na kiporo cha kuuanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba uliozaliwa na vikao vya maridhiano kati ya chama chake cha CCM na Chadema.

Katika moja ya hotuba zake, Rais Samia aliahidi kulitekeleza hilo kwa kuunda tume itakayohusisha watu wa makundi mbalimbali kuanza utekelezaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Machi 19, 2023 katika hafla ya maadhimisho ya miaka miwili tangu aapishwe kuwa mkuu wa nchi iliyofanyika Uwanja wa Uhuru, Rais Samia amesema atatekeleza takwa la Katiba mpya hatua kwa hatua.

"Kuna matakwa ya Katiba ibadikike tumesema sawa safari ni hatua tunakwenda hatua kwa hatua. Naahidi kwamba kwa sifa iliyojengwa na Tanzania ya utawala bora tunakwenda kutekeleza bila kupiga chenga yoyote ile.

"Nilisema mwanamke ni kujiamini nami kama Mwenyekiti wa CCM najiamini, najiamini kufungua uwanja wa siasa nikijua kwamba wana CCM tutakwenda pamoja na tutajadiliana na wenzetu na kuifanya nchi yetu twende vizuri," amesema.

Hata hivyo, amesema imani duni waliyokuwa nayo wengi kuhusu uwezo wake wa kuongoza kutokana na jinsia yake, ndiyo iliyompa chachu ya kufanya vema.

"Nilikuwa nafanya kazi kuhakikisha naonyesha kwamba nina uwezo wa kuongoza ili kupinga yale mabezo (kubezwa)," amesema.

Ameeleza kubezwa huko ndiyo siri ya juhudi za utendaji wake na hatimaye kila mmoja kwa sasa anasifu kinachofanywa naye.