RC Arusha akemea ma-DC wapya kukurupuka

Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Emmanuela Mtatifikolo akila kiapo cha utii leo Januari 31, 2023 jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema viongozi wanapaswa kuacha kufanya kazi kukurupuka na kuropoka kwani wakati mwingine wanaweza kuiabisha mamlaka na badala yake wajitafakari na kutumia hekima na utii pindi wanapotekeleza majukumu yao

Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amewaonya wakuu wapya wa wilaya kuacha kufanya kazi kwa kukurupuka na badala yake wazingatie kanuni na hekima na utiifu pindi wanapotekeleza majukumu yao.

Mongela amesema hayo leo Jumanne Januari 31, 2023 mara baada ya kuwaapisha wakuu wa Wilaya za Arusha, Longido na Arumeru.

Amesema kati ya masuala yanayomuudhi ni pamoja na watu kukurupuka na kuropoka kwani wakati mwingine wanaweza kuiabisha mamlaka na kuwataka kujitafakari kwa kina ili waweze kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.

"Nafasi hizi ni nzuri kama hekima itatumika. Hakuna kitu cha kishamba kinaniudhi kama watu kuropoka ropoka na kukurupuka kwa kudhani ndiyo ujanja.

"Tayari una dhamana watu wanajua wewe ndiye mjuu wa mkoa uko busy kutaka watu wajue wewe ndiye mkuu wa mkoa, kwani hatujui?

"Uko busy mimi ndiye Mkuu wa wilaya, tunajua na tulikuona unaapishwa sasa una wasiwasi gani? Unajitilia shaka kwamba unafikiri ukifanya maigizo labda ndiyo ukuu wa wilaya unakamilika au ukuu wa mkoa," ameongeza

Mongela amesema alivyosema kukurupuka hajamaanisha wawe kimya na badala yake wasimamie na kukemea masuala yanayohitaji kukemewa.

Walioapishwa ni Marko Ng'umbi (Longido), Felician Mtahengerwa (Arusha) na Emmanuela Mtatifikolo wa Arumeru.

Akizungumza katika hafla hiyo, Askofu Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, amewataka wakuu hao kutambua wana dhamana ya kusimamia na kuacha alama chanya katika maeneo yao.

"Uongozi ni vita, mtapigana na vita anaitwa rushwa ambaye mara nyingi hakamatwi, mtapigana na dawa za kulevya, mporomoko wa maadili, mna dhamana kubwa kusaidia jamii inayoteseka na kukabiliwa na changamoto mbalimbali," amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Emanuela amesema wanatambua mkoa wa Arusha ni muhimu katika sekta ya utalii na kuwa watahakikisha wanashirikiana na viongozi wengine kukuza sekta hiyo.

"Tunamshukuru Rais kwa kutuma imani na heshima hii kubwa na adhimu ya kumsaidia, tunamuahidi kufanya kazi kwa unyenyekevu, upendo na huruma kwa watanzania wenzetu na kutumika ipasavyo," amesema.