Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Babu atahadharisha mamluki uchaguzi serikali za mitaa

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amevionya baadhi ya vyama vya siasa mkoani hapa kuepuka kuleta mamluki kutoka nje ya maeneo yao kupigia kura akisisitiza 4R za Rais Samia Suluhu Hassan zitekelezwe katika uchaguzi huo.

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amevionya vyama vya siasa mkoani humo kuepuka kupeleka mamluki kutoka nje ya maeneo yao kupigia kura na kwamba wahakikishe 4R za Rais Samia Suluhu Hassan zinatekelezwa katika uchaguzi huo.

Babu ameyasema hayo Septemba 12, 2024 wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 ukihusisha vijiji 519, mitaa 60 na vitongoji 2,258.

Amesema kuelekea uchaguzi huo, mkoa umejipanga kuhakikisha katika matukio yote ya ratiba za uchaguzi kuanzia uandikishaji, uteuzi wa wagombea, kampeni za uchaguzi, upigaji kura na kutangaza matokeo, ulinzi na usalama unaimarishwa na hali ya utulivu na amani vinakuwepo.

“Hapa tumepakana na nchi jirani, sasa watu wanaochukua mamluki kutoka nchi jirani kutuletea huku sisi tumeshaikataa na nilishasema kwenye mkutano mmoja, kuna chama fulani hapa Moshi ili kishinde lazima kilete watu kutoka wilaya za karibu, nimeshasema kila mmoja akae kwenye eneo lake linalohusika,” amesema Babu.

Babu amesema kuanzia sasa ulinzi umeimarishwa mkoani humo mpaka siku ya kupiga kura Novemba 27 na matokeo yatakapotangazwa.

“Niwaombe wananchi wawe watulivu, wasikivu kipindi chote hiki na niwahakikishie kwamba tutaenzi na kuziishi kwa nguvu zetu zote 4R za Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi huu wa serikali za mitaa,” amesema Babu.

Ameongeza: “Sisi ndio waumini wa 4R za Rais, kwa hiyo kila tunapokwenda kwenye mikutano, kwenye semina nitazungumza na vyama vya siasa, tutawaambia dhamira ya Rais wetu kwamba katika uchuguzi huu, utakuwa ni wenye maridhiano, mashikamano na wenye utulivu uliopitiliza,” amesema RC Babu.

 “Wananchi watapata fursa ya kidemokrasia ya kuwachagua viongozi wao watakaoshirikiana nao katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika maeneo yao kwa kipindi cha miaka mitano,” amesema Babu.

Babu amesema wote watakaosimamia uchaguzi huo watapatiwa semina pamoja na mambo mengine na kwamba mtumishi yeyote wa serikali au aliyepewa dhamana ya kusimamia uchaguzi huo atakayevuruga uchaguzi huo atachukuliwa hatua za kisheria.

“Kwenye uongozi wangu sitaki kusikia dosari za uchaguzi, nataka nione mtu anachukua fomu anapanda jukwaani, ananadi sera zake na wananchi wanamsikiliza, kwa hiyo mtumishi yeyote wa Serikali au waliopewa dhamana ya kusimamia atakayetuvurugia uchaguzi huu, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema.

Naye, mratibu wa uchaguzi mkoani humo, Gasper Ijiko amesema wamejipanga vizuri kwenye uratibu wa shughuli zote za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unatekelezwa, kusimamiwa na kuratibiwa kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo.

“Tumejipanga vizuri kwa ajili ya kuratibu shughuli zote za uchaguzi, tunachokifanya sasa hivi ni maandalizi katika ngazi za msingi.

“Vituo vya kupigia kura maandalizi yake yanaendelea na tumeshafanya uhakiki na majina ya vituo yatakayoshiriki katika uchaguzi.

“Hakuna tukio ambalo litaendeshwa kienyeji, tunajipanga kuzingatia kanuni hizo, sisi tumejipanga kusimamia na kuzingatia kanuni maana nje ya kanuni utakuwa unafanya yako na uchaguzi haufanywi kwa matakwa ya mtu, bali kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, tumejipanga sana,” amesema Ijiko.

Hata hivyo, amewaomba wananchi kujiandaa kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo kikamilifu na kwamba utakuwa ni huru, wazi na shirikishi.

“Suala hili litakuwa ni shirikishi na kwa ushirikiano mkubwa na vyama vya siasa, kwa mujibu wa kanuni, watu wasiogope, wawe huru na kila kitu kitafuata sheria,” amesema Ijiko.