Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Babu awaomba wazawa kuwekeza hoteli Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

  • Kampeni hiyo ambayo inafanyika kwa mara ya tano mwaka huu, inalenga kuhamasisha Watanzania kupanda Mlima Kilimanjaro, kukuza utalii wa ndani na kuongeza mapato ya taifa.

Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewataka wawekezaji na wafanyabiashara wazawa wa mkoa huo kuwekeza zaidi katika sekta ya utalii kwa kujenga hoteli ili kukabiliana na wingi wa watalii wanaofika kupanda Mlima Kilimanjaro.

Akizungumza leo Julai 4, 2025, wakati wa uzinduzi wa msimu wa tano wa kampeni ya Twenzetu Kileleni, Babu amesema jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii zimefanikiwa, lakini changamoto ya uhaba wa hoteli bado ni kubwa.

“Rais amefanya kazi kubwa ya kukuza utalii na leo tunapata wageni wengi, lakini hatuna pa kuwaweka. Hoteli zimejaa, hadi baadhi ya watalii wanalazimika kwenda kulala Arusha,” amesema Babu na kuongeza:

“Wengi wanawekeza Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, lakini hapa kwao wanapakimbia. Natamani kuona wawekezaji wetu wakirudi nyumbani kuwekeza. Fursa ni kubwa.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Zara Adventures, Zainab Anselim, amesema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha Watanzania kupanda Mlima Kilimanjaro na kukuza utalii wa ndani, huku msimu huu wakitarajia kupandisha zaidi ya watu 250.

“Hii ni kampeni ya uzalendo kwa Watanzania kuenzi mlima wao. Tunawakaribisha wote waje kupanda mlima wetu, ambao umepewa tuzo ya ‘The Best Mountain in the World’,” amesema Zainab ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika biashara ya utalii.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Angela Nyaki, amepongeza kampeni hiyo na kufichua kuwa kwa mwaka huu, njia zaidi za kupandia mlima zimeongezwa, huku safari za siku moja hadi tatu pia zikiruhusiwa kwa wasio na uwezo wa kupanda hadi kilele.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kukuza utalii wa ndani ili kuongeza mapato na kutoa ajira kwa vijana.

“Mlima Kilimanjaro ni paa la Afrika, tutaendelea kuhakikisha unaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya taifa na fursa kwa Watanzania,” amesema Mnzava.