RC Dendego afungua milango kushughulikia kero za mafundi Iringa
Mkurugenzi wa FundiSmart, Fredy Herbet akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego kuzungumza na mafundi. Pembeni ni meneja wa kampuni hiyo, Fabian Mwiga.
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ametumia Kongamano la Mafundi Iringa kuwataka waunde vikundi kulingana na aina yao ya ufundi ili iwe rahisi kusikiliza kero zao na kushughulikia.
Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amewataka mafundi kuunda vikundi na kupata uongozi ili iwe rahisi kukutana nao, kuwasikiliza, kutatua kero na kuandaa mkakati utakaowasaidia kupiga hatua kiuchumi.
Akizungumza jana Machi 17, 2023 katika Kongamano la Mafundi Iringa lililoandaliwa na Kampuni ya FundiSmart, Dendego amesema sio rahisi kushughulikia kero za mafundi hao ikiwa hawajaamua kuungana.
“Kongamano hili litumike kuandaa vikosi kazi, pateni uongozi ili nikija tukae na kuona mnawezaje kupata fursa,” amesema Dendego.
Amewataka mafundi kuwa waaminifu kwenye kazi zao ili iwe rahisi kupiga hatua kiuchumi.
Awali, Mkurugenzi wa FundiSmart, Fredy Herbet amesema hakuna namna mafundi wanaweza kutoboa kiuchumi bila kupambana katika kuhakikisha wanabadilisha mtizamo wa jamii juu yao.
“Hata kama ungekuwa fundi mahiri kiasi gani bila kufuata misingi ya kazi hiyo sio rahisi kutoboa, lazima tubadilike na kuwa waaminifu kwenye kazi za watu na tujitachangamoto zetu mafunzi tuzitumie kama fursa ya kufika mafanikio yetu,” amesema Herbat.
Kwa upande wao baadhi ya mafundi wamekiri kuwepo na mtazamo hasi kuhusu kazi zao jambo ambalo linawafanya wengi wabaki maskini.
Fundi gereji wa Kihesa, Manispaa ya Iringa, Joshua Koli amesema pande zote mbili baina yao na wateja wamekuwa sababu kubwa ya kazi hiyo kuonekana haina manufaa kwao.
“Anakuja mteja, anataka umfanyie kazi kwa ujira mdogo kabisa, hapo unawatoto na familia nzima inakutegemea unadhani utakataa? Hapana, unapokea zote ili upambane kumaliza pesa iongezeke, matokeo yake ni kutomaliza kwa wakati,” amesema.
Meneja wa FundiSmart, Fabian Mwiga amesema kongamano la Iringa ni la tatu likitanguliwa na lile la Mbeya na Dodoma.
“Kongamano lijalo litafanyika Mkoani Mwanza na lengo kubwa ni kuwasaidia mafundi katika kuwapatia elimu ya afya, usalama mahali pa kazi, sheria, huduma bora kwa wateja na fedha,” amesema Mwiga.