RC Kagaigai apigia debe uwekezaji Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai akizungumza na viongozi wa dini(hawapo Pichani)katika ukumbi mdogo wa ofisi hizo.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amezitaka taasisi mbalimbali zikiwemo za dini kuwekeza mkoani humo kwa lengo la kuendeleza sera ya viwanda ili kukuza zaidi uchumi.
Moshi.Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amezitaka Taasisi mbalimbali zikiwemo za dini kuwekeza mkoani humo kwa lengo la kuendeleza sera ya viwanda ili kukuza zaidi uchumi.
Amesema yapo maeneo mengi ya wazi yaliyotengwa na Serikali katika halmashauri za mkoa huo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kagaigai ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 27,2021 mara baada ya kukutana na viongozi wa dini mkoani humo kwa lengo la kufahamiana na kujadiliana changamoto zilizopo Kilimanjaro.
"Mkoa wa Kilimanjaro ni wetu sote na nyie ni wadau wakubwa wa maendeleo ,tunavyokutana hivi tunajenga uhusiano wa kujua changamoto zinazotukabili katika shughuli zetu ,"
"Najua baadhi ya Taasisi zenu zimewekeza katika elimu na maeneo mengine lakini niwahimize kwa zile ambazo ziko tayari kuwekeza tuna maeneo mengi yaliyotengwa na Serikali katika halmashauri zetu kwa ajili ya uwekezaji na mengi nimeambiwa yako wazi, njooni muwekeze ,"amesema Kagaigai
Amesema yuko tayari kusikiliza kero zote ambazo wanajua ni kikwazo kwao cha kufanya mambo ya maendeleo ili aweze kuwasaidia.
"Sasa hivi tuko kwenye uchumi wa viwanda, mimi niko tayari mnieleze kwamba mnawekeza lakini kuna vikwazo moja mbili tatu ili niwasaidie,"amesema Kagaigai