RC Kagaigai ataka ushirikiano Kilimanjaro
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa mkuu wa Mkoa huo, Anna Mghwira.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wakuu wa wilaya, watendaji wa halmashauri pamoja na wakuu wa idara kufanya kazi kama timu ili kuleta ufanisi.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka wakuu wa wilaya, watendaji wa halmashauri pamoja na wakuu wa idara kufanya kazi kama timu ili kuleta ufanisi.
Kagaigai ameyasema hayo leo Jumanne Mei 25, 2021 katika makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Anna Mghwira.
Amewataka wananchi kumpa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza yanayokusudiwa na Serikali.
“Rais amenileta huku nimsaidie kutekeleza ilani ya CCM katika kuwatumikia wananchi, ninapenda kufanya kazi kama timu, ofisi yangu kila siku itakuwa wazi ili mtu yeyote mwenye shida na matatizo nimwone na nimsikilize tuone namna ya kutatua changamoto zake.”
“Nawaomba sana wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri pamoja na watendaji wote wanisaidie kwa maana ya kuacha ofisi zao wazi ili waweze kuwapokea wananchi na kusikiliza kero zao na kuzitatua. Huu Mkoa nataka tuutendee haki, ni mkoa wetu sote kwa hiyo sitawaangusha wananchi nawaahidi kuwatumikia,” amesema.