RC Kagaigai atoa maagizo Same
Muktasari:
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Stephen Kagaigai ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same kukamilisha vituo vya afya vya Mtii na Miyamba ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Same. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Stephen Kagaigai ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Same kukamilisha vituo vya afya vya Mtii na Miyamba ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Vituo hivyo ambavyo vimetengewa Sh750 milioni na Serikali vitasaidia kuhudumia zaidi ya wananchi 20,000 ambao hulazimika kutembea zaidi ya kilomita 18 kutafuta huduma za afya.
Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo, RC Kagaigai amewataka makandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo hivyo vikamilike kwa wakati.
"Vituo hivi vya afya vya Miyamba na Mtii vinahitajika kwa haraka na ikifika mwezi Juni mwaka huu kama mlivyoniahidi viwe vimekamilika ili wananchi wa maeneo haya waanze kupata huduma katika kituo hiki. Tayari Serikali imeshatoa Sh750 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huu, sioni sababu ya kuchelewesha ujenzi huu," amesema Kagaigai
"Wananchi tunaomba muendelee kuwa na subira, kituo hiki kitakamilka mapema, niwaombe wataalamu wote mliopewa nafasi ya kusimamia ujenzi huu mharakishe."
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same (DC), Edward Mpogolo amesema vituo hivyo vitaweza kuwahudumia zaidi wananchi 20,000 ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 18 kusaka huduma za afya.
Baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakipata changamoto za upatikanaji wa huduma za afya kwa karibu hali ambayo imekuwa ikiwatesa kwa muda mrefu na wakati mwingine kupoteza wapendwa wao kwa ucheleweshwaji wa huduma.