RC Kagaigai awataka CCM, Serikali kusimamia miradi ya maendeleo
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka viongozi wa Serikali na CCM kuanzia ngazi za vijiji, vitongoji na kata mkoani humo kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayotolewa na serikali.
Same. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amewataka viongozi wa Serikali na CCM kuanzia ngazi za vijiji, vitongoji na kata mkoani humo kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi ya maendeleo inayotolewa na serikali.
Ameyasema hayo leo Novemba 11, 2021 wilayani Same wakati akizungumza na watendaji wa vijiji, vitongoji, kata pamoja na makatibu wa mashina wa CCM katika semina ya kuwakumbusha watendaji hao uelewa wa majukumu yao.
"Ni muhimu ninyi viongozi mkajiona ni sehemu ya mipango ya miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali yetu, kwa misingi hiyo mnatakiwa muwe mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa maendeleo kwenye maeneo yenu.
"Mkiona kuna kitu hakiendi sawa kwenye hii miradi mnajukumu la kutoa taarifa kwa viongozi wa juu zaidi ili lifanyiwe kazi, ninyi mna dhamana kubwa ya kusimamia maendeleo kwenye maeneo yenu," amesema RC Kagaigai.
Pamoja na mambo mengine ametembelea baadhi ya shule za wilaya hiyo kuangalia shughuli za ujenzi wa madarasa unaoendelea wilayani humo ambapo amepongeza kasi ya ujenzi wa madarasa hayo.