RC Kilimanjaro atoa maagizo ujenzi jengo la mama na mtoto Mawenzi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amemwagiza mkandarasi anayesimamia mradi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Rufaa Mawenzi kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliopangwa.
Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amemwagiza mkandarasi anayesimamia mradi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali ya Rufaa Mawenzi kukamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliopangwa.
Kagaigai ametoa maagizo hayo leo Jumatano Oktoba 27, 2021 alipofanya ziara ya kukagua shughuli za ujenzi zinazoendelea katika hospitali hiyo amesema Serikali imetoa Sh3 bilioni kwa ajili ya kumaliza ujenzi huo.
Hadi sasa jengo hilo limegharimu zaidi ya Sh6 bilioni.
Aidha amemuagiza katibu tawala wa mkoa huo, Dk Seif Shekalage kusimamia manunuzi kwa ajili ya ujenzi huo ili jengo hilo liweze kukamilika kwa wakati na kwa muda uliopangwa wa miezi minne na siku tano.
"Nikupongeze kwa namna unavyofuatilia, mara ya kwanza nilipotembelea jengo hili niliambiwa lina miaka 12 bado halijakamilika niliumia sana kwa sababu jengo hili linatakiwa lihudumie mama na mtoto,"amesema Kagaigai
"Namshukuru Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia jengo hili,niwaombe wakandarasi mnaosimamia ujenzi huu ule utaratibu niliokuta kipindi kile sitaki kuuona tena, nataka ujenzi huu uende kwa spidi hili jengo likamike kwa wakati uliopangwa," amesema Kagaigai.