Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Lindi aitaka Takukuru kuimarisha usimamizi wa miradi

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, akisisitiza jambo wakati wa warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Lindi. 

Muktasari:

  • Miradi ya Sh300 bilioni imekaguliwa na Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Lindi, huku miradi 22 ilikutwa na kasoro na miradi 137 ikiwa na mapungufu na ilielekezwa kutekelezwa upya.

Lindi. Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ameielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za manunuzi ya umma zinafuatwa ili kuondoa ucheleweshaji na utekelezaji wake.

Telack ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Julai 15, 2026, alipokuwa akifungua warsha ya siku moja ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Takukuru Mkoa wa Lindi kwa lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Amesema usimamizi madhubuti wa miradi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha fedha za Serikali zinaleta matokeo yaliyokusudiwa na wananchi wanapata huduma bora zinazotokana na uwekezaji wa umma.

"Warsha hii ni muhimu kwa sababu inaongeza ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali katika kuzuia rushwa na kuimarisha uwajibikaji. Usimamizi mzuri wa rasilimali za umma utahakikisha fedha za Serikali zinatumika ipasavyo kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo yenye tija," amesema Telack.

Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Lindi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo, Zainab Telack, alipokuwa akizungumza katika warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Lindi.

Aidha, ameitaka taasisi hiyo kuendelea kufuatilia mchakato wa ununuzi wa umma ili kuhakikisha makandarasi wanaopewa zabuni wanakuwa na sifa, uwezo na uzoefu wa kutekeleza miradi kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Lindi, Stephen Mafipa amesema taasisi hiyo imekagua miradi 159 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh300 bilioni katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 hadi 2025/26.

Amesema ukaguzi huo umebaini miradi 22 ilikuwa na kasoro zilizohitaji kurekebishwa, huku miradi 137 ikionekana kuwa na upungufu uliosababisha kutolewa kwa maelekezo ya kutekelezwa upya kwa kuzingatia taratibu na viwango vinavyotakiwa.

"Matokeo haya yanaonyesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo. Tunawahimiza watumishi wa umma na wadau wote kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji ili miradi hiyo itoe manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi," amesema Mafipa.

Amesisitiza kuwa Takukuru itaendelea kushirikiana na taasisi za Serikali na wadau wengine kuhakikisha mianya ya rushwa inazibwa na fedha za umma zinalindwa kupitia usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo.

Warsha hiyo imewakutanisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama, watumishi wa umma pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.

Wamejadili namna ya kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo na kuzuia vitendo vya rushwa vinavyoweza kuathiri utekelezaji wake.