Takukuru yaibua udhaifu miradi ya maendeleo Morogoro
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Pilly Mwakasege
Muktasari:
- Taasisi yabaini miradi kuchelewa, wananchi kutoshirikishwa na kasoro za usimamizi wa fedha za umma. Baadhi ya miradi iliyogharimu mamilioni ya shilingi imekamilika bila kuanza kutoa huduma kutokana na mapungufu ya utekelezaji. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima atoa onyo kwa wasimamizi wa miradi kuhakikisha uwajibikaji.
Morogoro.Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Morogoro imebaini upungufu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwamo baadhi kukamilika lakini kushindwa kutoa huduma zilizokusudiwa, ucheleweshaji wa utekelezaji na wananchi kutoshirikishwa katika hatua muhimu za uanzishaji na usimamizi wa miradi hiyo.
Akizungumza katika warsha ya wadau wa usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanyika Julai 10, 2026 mjini Morogoro, Mkuu wa Takukuru Mkoa huo, Pilly Mwakasege, amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miradi ya maendeleo unahitaji usimamizi madhubuti ili kuhakikisha fedha hizo zinatoa thamani iliyokusudiwa.
Amesema udhaifu wa usimamizi pamoja na vitendo vya rushwa vinaweza kusababisha miradi kujengwa chini ya viwango, kuongezeka kwa gharama zisizo za lazima, kuchelewa kukamilika kwa miradi na wananchi kukosa huduma zinazotarajiwa.
“Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia thamani ya fedha,” amesema Mwakasege.
Amesema kupitia ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma (PETS), Takukuru imebaini viashiria vya uvujaji wa rasilimali, ushiriki mdogo wa wananchi katika miradi pamoja na changamoto za usimamizi zinazochangia baadhi ya miradi kutofikia malengo yake.
Ameongeza kuwa baadhi ya mapungufu hayo yamekuwa yakijirudia licha ya kuwepo kwa maelekezo mbalimbali kutoka kwa viongozi kuhusu umuhimu wa usimamizi bora wa miradi.
Miradi yashindwa kuanza kazi
Akiwasilisha mada katika warsha hiyo, Mkuu wa Dawati la Kuzuia Rushwa wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Happiness Munisi amesema uchunguzi wa taasisi hiyo umebaini baadhi ya miradi iliibuliwa na kutekelezwa bila kuwashirikisha wananchi ambao ndio walengwa wakuu.
Amesema kutoshirikishwa kwa wananchi tangu hatua za mwanzo kumesababisha baadhi ya miradi kushindwa kutumika baada ya kukamilika.
Ametolea mfano Soko la Kata ya Lundi, Wilaya ya Morogoro, ambalo limekamilika lakini bado halijaanza kutoa huduma kutokana na changamoto za ushirikishwaji wa wananchi katika hatua za awali za mradi.
Munisi pia ametaja kituo cha utalii kilichojengwa Kijiji cha Kinole kwa gharama ya takribani Sh45 milioni, akisema hakijafikia malengo yaliyokusudiwa kutokana na wananchi kutohusishwa kikamilifu wakati wa kuibua wazo la mradi huo.
Aidha, amesema taasisi hiyo ilibaini kasoro katika usanifu wa Shule ya Msingi Kilongo, ambapo milango ya madarasa ilijengwa tofauti na vipimo vilivyoainishwa kabla ya wahandisi kufanya marekebisho.
Mapungufu miradi ya elimu
Munisi amesema ufuatiliaji wa miradi ya BOOST, SEQUIP na Amali umeonyesha kuwepo kwa changamoto katika uundaji wa kamati za utekelezaji pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za vifaa vya ujenzi.
Pia amesema mradi wa ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Kiroka ulichelewa kuanza kwa miezi minne licha ya fedha za utekelezaji kuwa zimetolewa.
Hata hivyo, amesema hatua zilizochukuliwa kutokana na ufuatiliaji wa Takukuru zimewezesha baadhi ya miradi kufanyiwa maboresho, akitaja Daraja la Fungafunga ambalo lilifanyiwa marekebisho baada ya mapendekezo ya taasisi hiyo.
RC atoa onyo
Akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adams Malima amesema Serikali imeendelea kuelekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, hivyo fedha hizo hazipaswi kupoteza thamani kutokana na uzembe au udhaifu wa usimamizi.
Amewataka viongozi, watendaji na wasimamizi wa miradi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji bila kusubiri taasisi za nje kubaini mapungufu katika maeneo yao.
“Ni lazima tujifunze kutokana na makosa yaliyopita, tusiruhusu yarudiwe na tuhakikishe kila mradi unakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na unatoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi,” amesema Malima.
Amesema usimamizi bora wa miradi ya maendeleo utaongeza imani ya wananchi kwa Serikali, kulinda fedha za walipa kodi na kuchochea kasi ya maendeleo katika Mkoa wa Morogoro.