RC Mbeya amwagiza RPC kukamata magari

Majeneza sita yaliyohifadhi miili ya wafanyakazi sita wa Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ikiagwa katika viwanja vya kituo cha afya igawilo jijini Mbeya leo Oktoba 25,2021 picha ba Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amemuagiza Kamanda wa Polisi mkoani humo, Urlich Matei kukamata madereva wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani bila kujali iwapo ni madereva wa magari ya Serikali au la.

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amemuagiza Kamanda wa Polisi mkoani humo, Urlich Matei kukamata madereva wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani bila kujali iwapo ni madereva wa magari ya Serikali au la.


Homera ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Novemba 25, 2021 alipoongoza mamia ya wakazi jijini Mbeya na viongozi wa Serikali kuaga miili ya wafanyakazi sita wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kituo cha Wilaya ya Mbarali mkoani humo.


Miili hiyo imeagwa katika viwanja vya kituo cha afya Igawilo na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo ndugu na jamaa wa marehemu.


"RPC Fanya uparesheni ya kukamata madereva wote wanaokiuka sheria za usalama barabarani  pasipo kujali magari ya Serikali kama STL wala  STJ kwani sio jambo jema kukiuka sheria za barabarani kwasababu zisizo na msingi na hivyo kugharimu maisha ya watanzania "amesema.


Aidha Homera ametoa salamu za pole kwa wafiwa kwa niaba ya Serikali na kwa kupoteza vijana ambao walikuwa tegemeo kwa taifa katika kuchochea shughuli za miradi ya maendeleo hususan nishati ya umeme.


Naye Naibu Spika na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi walioshiriki ibada hiyo amewatia moyo ndugu na jamaa waliopoteza wapendwa wao.


Oktoka 23, 2021 majira ya saa 11 jioni katika eneo la Inyala wilaya ya Mbeya wafanyakazi sita  wa Tanesco Wilaya ya Mbarali walipoteza maisha na wengine 12 kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya Rufaa ya kanda  baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka.


Miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na , Swanini Kilumile(26), Physon Maeda (33), Prisca Mwalongo (26), Silvano Baraka (27), Samuel Lusingu (31) na Sarehe Hamis (36) ambapo kati ya majeruhi 12 wawili waliruhusiwa.