RC Mongela awataka wabunifu Arusha kufika soko la nje

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amewataka wabunifu mkoani humo kutoishia kwenye tafiti pekee bali waende  mbali zaidi katika kuzalisha kwa wingi bidhaa ili kuyafikia masoko ya ndani na nje ya nchi.


Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amewataka wabunifu mkoani humo kutoishia kwenye tafiti pekee bali waende  mbali zaidi katika kuzalisha kwa wingi bidhaa ili kuyafikia masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameyasema hayo leo Jumanne Mei 10, 2022 jijini Arusha kwenye wiki ya Ubunifu 2022 kwa mkoa huo ikiwa ni sehemu ya wiki ya Ubunifu nchini itakayofanyika Jijini Dodoma Mei 15 inayoenda na kauli mbiu "Ubunifu kwa maendeleo endelevu".

Amesema kuwa, ipo haja kwa wabunifu nchini kuacha kujikita katika tafiti pekee na kuanza utengenezaji wa bidhaa walizobuni kwa wingi ili kuyafikia masoko hilo litakuwa jambo litakalosaidia ukuaji wa maendeleo.

"Niwaombe sana sisi Serikali ya mkoa tutatoa eneo kwa ajili ya kufanya mkoa wa Arusha kuwa kitovu cha Ubunifu nchini ili kuendeleza tafiti ambazo zimeshabuniwa kuweza kuleta tija na kuinua uchumi"amesema Mongela.

Naye, Mkurugenzi wa programu wa  Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC), Sara Teri amesema msingi wa ushiriki wao umejikita katika dhana nzima ya kijana anashiriki vipi katika ajira na uongozi ili kuweza kuwasilisha kwa serikali katika kusaidia utungaji sera.

Amesema kuwa wao kama chuo ni jukumu lao kusaidia vijana katika mambo ya ubunifu ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kutambua wajibu wao kwa lengo la kukuza Ubunifu

Kwa Upande wake Collins Kimaro, Meneja Mkuu wa Westerwelle startup Haus Arusha amewataka wabunifu nchini kushiriki na kujiuliza swali la kauli mbiu ya wiki hiyo kuona wanaibadilisha vipi fikra kuwa fursa za kukuza Ubunifu nchini.