RC Mtaka apiga marufuku uhamisho walimu
Mkuu wa mkoa wa Njombe (RC), Anthony Mtaka
Muktasari:
Mkuu wa mkoa wa Njombe, Antony Mtaka amesema walimu wanatakiwa kukumbuka nyuma na kumshukuru Mungu kwa nafasi za ajira walizozipata sasa licha ya kuhangaika kwa muda mrefu.
Njombe. Mkuu wa mkoa wa Njombe (RC), Anthony Mtaka amepiga marufuku kutoa vibali vya uhamisho kwa walimu wa ajira mpya huku akiwataka wafanye kazi katika vituo walivyopangiwa kwa uadilifu.
Mtaka ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Septemba 12, 2022 katika kikao maalumu cha kujadili uboreshaji elimu ya msingi na sekondari kilichofanyika mkoani humo.
Amesema wapo walimu ambao wamemwomba Mungu kwa muda mrefu ili wapate ajira na hatimaye Mungu akasikia kilio chao lakini siku chache baadaye wanaanza kutoa visingizio ili wahamishwe kituo cha kazi.
“Wakati unaomba kazi kwenye mfumo hukujua shule unayoenda, ulikuwa unaomba Mungu nisaidie nipate ajira, hivyo sitarajii mtu mwingine mjinga akamfuata ofisa elimu kumwambia nihamishie kituo fulani,” amesema Mtaka.
Mkuu huyo wa mkoa amesema walimu wanatakiwa kukumbuka ya nyuma kwa kushukuru nafasi ya ajira walizozipata sasa licha ya kuhangaika kwa muda mrefu.
Amesema maelfu ya watu ambao wamehitimu elimu ya chuo kikuu ngazi ya shahada wapo mitaani lakini hawajafanikiwa kupata ajira.
Mtaka amesisitiza kwamba hakuna simu yoyote kutoka kwa mtu ambaye inaweza kusababisha mwalimu wa ajira mpya kuweza kubadilishiwa kituo cha kazi mkoani hapa, vinginevyo aache kazi.
Ameongeza kwamba kuna shida ya baadhi ya watu kushindwa kutambua sehemu wanazotoka kwa kuomba kazi kwa muda mrefu huku wakitoa maneno yasiyofaa mtandaoni lakini wakiipata wanaanza kuichezea.
Amewataka maofisa elimu mkoani humo kutojaribu kufanya uhamisho wa mwalimu kutoka kituo alichopangiwa na kwenda kingine.
Amesema mikakati iliyopo ni kuinua kiwango cha elimu kuanzia ngazi za halmashauri, wilaya, mkoa na kitaifa kwa kuondoa sifuri katika shule zote za mkoa wa Njombe.