RC Songwe awatangazia kiama maofisa ardhi

Katibu wa Kamati iliyoundwa kuchunguza uharibifu wa mazingira na chanzo cha migogoro ya ardhi mkoani mkoani Songwe, Maulid Mpanye kushuto akikabidhi ripoti kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba. Picha na Stephano Simbeye.
Muktasari:
Kamati ya watu nane iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa Songwe, Omary Mgumba Februari 2022 kuchunguza uharibifu wa mazingira na chanzo cha migogoro ya ardhi mkoani humo imewasilisha ripoti yake na mapendekezo huku hatua za kinidhamu zikiagizwa zichukuliwe kwa wahusika.
Songwe. Kamati ya kuchunguza uharibifu wa mazingira na migogoro ya ardhi mkoani humo, imebaini umilikishaji ardhi usiofuata sheria na utoaji holela wa vibali vya kusafisha mashamba ni baadhi ya vyanzo vya migogoro ya ardhi na uharibifu wa mazingira katika mkoa huo.
Kamati hiyo ya watu nane iliyoundwa Februari 2022 na Mkuu wa Mkoa Songwe (RC), Omary Mgumba kuchunguza uharibifu wa mazingira na chanzo cha migogoro ya ardhi mkoani humo.
Katibu wa kamati hiyo, Maulid Mpanye akikabidhi riporti hiyo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Songwe leo Jumamosi Julai 23, 2022 amesema kumekuwa na umilikishaji ardhi usiozingatia sheria na utoaji holela wa vibali vya kusafisha mashamba bila kuzingaria athari za kimazingira.
Amesema hiyo ni miongoni mwa sababu zilizochangia kuwepo na migogoro mingi ya ardhi kati ya vijiji na vijiji ikiwemo watu zaidi ya mmoja kupewa kiwanja kimoja.
Kamati hiyo imebainisha sababu nyingine ni tafsiri mbaya ya tangazo la Serikali (GN No.419) iliyotolewa mwaka 2019 ambayo inatoa mwanya wa uharibifu wa mazingira kwa kutoa kibari cha kumilikisha ekari 13000 kwa pamoja kinyume na sheria ya ardhi ya vijiji namba 4 na 5 ya mwaka 1999.
Mpanye amesema kamati yake inashauri Serikali kunywang'anya hati za watu waliopewa ardhi kinyume na sheria na kuwachukulia hatua maofisa ardhi waliohusika kutoa ardhi hizo huku wakijua wanavunja sheria husika.
Jambo lingine ambalo kamati hiyo imeshauri ni zuio la uchomaji mkaa lililowekwa na Serikali mkoani hapa liendelee na kuongeza nguvu.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, RC Mgumba amemwagiza Katibu Tawala Mkoa huo, Mesaile Musa kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria maofisa ardhi waliokiuka taratibu za umilikishaji ardhi kwa kutumia vibaya sheria ya ardhi ya vijiji.
Mgumba ameagiza vyombo vinavyohusika kuanza mara moja uchunguzi kwa wale wote waliotajwa katika ripoti hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe pasipo kumwonea mtu.