RC Tabora ataja sababu wakulima kukosa mbolea

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dk Batilda Burian, mwenye ushungi, akiwa na wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya siku ya mbolea Duniani. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Kutokana na kutopata ruzuku wakulima zaidi ya laki moja mkoani Tabora msimu uliopita .mkoa kutumia maadhimisho ya siku mbolea duniani kutoa elimu kwa wakulima.

Tabora.  Zaidi ya wakulima 120,000 sawa na asilimia 80.6 hawajanufaika na mbolea ya ruzuku mkoani Tabora msimu uliopita huku wakulima 29,517 sawa na asilimia 19.3 wakinufaika na mbolea hiyo.

Akizungumzia maadhimisho ya siku ya mbolea duniani yanayotarajiwa kufanyika Kitaifa mkoani Tabora kuanzia Oktoba 11 hadi 13 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amesema wakulima ambao hawajanufaika ni kutokana na umbali uliokuwepo katika kufuata mbolea na ukosefu wa elimu kuhusu mbolea hiyo ya ruzuku.

Amesema mkoa utatumia maadhimisho hayo kutoa elimu kwa wakulima pamoja na kuongeza vituo vya usambazaji mbolea za ruzuku kutoka 16 msimu uliopita hadi 80 msimu huu.

"Ukiacha ukosefu wa elimu ya mbolea ya ruzuku umbali nao umechangia wa wakulima kuifuata mbolea hiyo ambapo kulitakiwa matumizi makubwa ya rasilimali fedha," amesema

Ameeleza kuwa msimu huu mahitaji ni tani 60,000 za mbolea ambapo tani 32,000 ni za tumbaku na tani 28,000 ni za mazao ya mahindi,alizeti na mazao mengine.

Kupitia wakulima 29,517 walionufaika na mbolea ya ruzuku kiasi cha tani 8,002 zilitumika kwa kutumia Sh8.5 bilioni.

Dk Batilda Burian amesema katika maadhinisho hayo siku mbili za kwanza zitahusisha maonesho kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya Kilimo hususan mbolea wakiwemo wazalishaji wa mbolea, zikiwemo kampuni  zaidi ya 15 zinazoingiza na kusambaza mbolea,mashirika na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo sanjali na Taasisi za Fedha.

Ameleeza lengo la maadhimisho hayo kuwa ni kupanua wigo zaidi wa kuelezea masuala mbalimbali katika mbolea ikiwemo mafanikio yake nchini na kutoa elimu kwa wadau wa mbolea hususan wakulima na wafanyabiashara wa mbolea.

Naye Abdallah Mkwaju mkazi wa Kitete Manispaa ya Tabora amesema anataka kupata elimu ya matumizi ya mbolea kwa mazao yake ya karanga,mihogo na mahindi sanjali na kufahamu dawa sahihi za kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao hayo.

Maadhimisho hayo yanatarajia kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dk Batilda Burian Oktoba 11, 2023 na kufungwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bshe Octoba 13, 2023.