RC Tanga: Wawekezaji wasiolipa fidia wanyang’anywe ardhi
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa amesema ana taarifa za baadhi ya wilaya kuwa na wawekezaji waliotakiwa kulipa fidia Sh400 milioni kwa wananchi takribani, lakini wameshindwa kulipa huku wakiendelea kushika ardhi ya wananchi.
Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha maeneo ya ardhi yaliyotolewa kwa wawekezaji ambao wameshindwa kulipa fidia kwa wananchi yanarudishwa.
Agizo hilo amelitoa leo Ijumaa, Septemba 13, 2024 wakati wa kufungua kikao cha Baraza la Biashara la mkoa.
Batilda amesema kuwa baadhi ya wawekezaji wamechukua maeneo ya wananchi lakini wameshindwa kulipa fidia, jambo ambalo linatishia kusababisha migogoro.
Ameongeza kuwa kushindwa kulipa fidia kunaashiria kwamba hata uendeshaji wa miradi ya wawekezaji hao unatia mashaka.
Ameagiza kuwa wale wote ambao hawajakamilisha masharti ya fidia warudishe ardhi hiyo ili itumike kwa shughuli nyingine za maendeleo.
Amesema kuna baadhi ya wawekezaji ambao wanadaiwa takribani Sh400 milioni kama fidia kwa wananchi lakini hawajafanya malipo hayo.
Ofisa Uwekezaji Mwandamizi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Valentine Vedasto, ameeleza kuwa sheria za uwekezaji nchini zinaruhusu kupokonywa ardhi kwa mwekezaji ambaye ameshindwa kutekeleza masharti ya uwekezaji.
Amesema ikiwa ni mwekezaji mkubwa, mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi inabidi itekelezwe na Rais, huku kwa ardhi ya ngazi za kijiji, hatua hizo zinaweza kuchukuliwa na mamlaka husika za kijiji au wilaya.
“Kama ardhi iliyopo kwenye ngazi ya kijiji, itategemea ni utaratibu gani mwekezaji amepatiwa, lakini kama hajawekeza chochote hadi inatokea hali hiyo kwa utaratibu wa sheria za TIC, kuna sababu ya kumnyang’anya ardhi husika,” amesema Vedasto.
Wakati huohuo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Peter Milanzi, amesema bandari hiyo inahitaji maeneo zaidi ya ardhi kwa ajili ya kuwekeza bandari kavu ili kusaidia kupokea mizigo kutokana na ongezeko la meli zinazoingia bandarani.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Tanga, Hadija Tingi, ameeleza kuwa uwanja huo utaanza kufanyiwa matengenezo makubwa mwezi huu, ikijumuisha upanuzi wa njia ya kuruka ndege, banda la abiria, maegesho ya ndege, na uzio wa kuimarisha ulinzi.
Miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea mkoani Tanga, ambapo kwa ujumla inagharimu Sh2.8 trilioni, huku Sh1.2 trilioni zikielekezwa kwenye miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa bomba la mafuta na mradi wa maji wa miji 28.