Ridhiwan akabidhi msaada wa madawati 390

Ridhiwan akabidhi msaada wa madawati 390

Muktasari:

  • Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete  amemkabidhi  Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, madawati 390 yenye thamani ya Sh30 milioni ili kupunguza tatizo la uhaba wa madawati lililopo katika shule za Chalinze.

Chalinze.  Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete  amemkabidhi  Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, madawati 390 yenye thamani ya Sh30 milioni ili kupunguza tatizo la uhaba wa madawati lililopo katika shule za Chalinze.

Shule za sekondari zilizopo chalinze zinakabiliwa na uhaba wa walimu na upungufu wa madawati ambavyo vinaathiri utoaji wa elimu katika shule hizo.

Kunenge amepokea madawati hayo leo, Alhamisi Mei 27, 2021 alipokuwa kwenye ziara ya kujitambulisha kwa watendaji na baraza la madiwani wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madawati hayo, Ridhiwan amesema jimbo hilo lina upungufu mkubwa  wa walimu wa sekondari wa masomo ya sayansi ambapo wanahitajika 118 na wa arts 15.

Amesema kuwa kulikuwepo na mahitaji ya madawati 754 na baada ya kukaa na kamati ya mfuko wa jimbo wakakubaliana kusaidia sehemu ya hitaji hilo na kufanikisha kupata dawati hizo 390 .

Ridhiwani ameeleza kuwa madawati hayo yatapelekwa kwenye shule 13 za sekondari ili wanafunzi wajifunze wakiwa wamekaa na hivyo wanaweza kufanya vizuri na kuongeza ufaulu.

"Mkuu wa mkoa, ninasikitika kusema kuwa halmashauri yetu tumekuwa tukifanya vizuri sana katika maeneo mengine ya ukusanyaji mapato na miradi ya maendeleo lakini kwenye eneo la elimu hatufanyi vizuri na nadhani ni kutokana pia na changamoto hii ya madawati hivyo leo tunapambana kuiindoa , tutashukuru ukituunga mkono "amesema Ridhiwani.

Naye Mkuu wa mkoa Abubakar Kunenge akipokea madawati hayo ameahidi kushirikiana na halmashauri ya Chalinze kuondoa kero ya madawati.

Amesema wananchi wana kero zinazowakabili na kwamba wanataka ziondolewe hivyo ni wajibu wa watumishi kutekeleza wajibu wao na kila mmoja kuona kero zilizopo ni sehemu yake kuzitatua.

"Tujiulize tatizo ni nini, alilolisema Ridhiwani hapa ndio kauli ya wananchi kwa sababu yeye ni mwakilishi wao, ni mwakilishi wa wazazi anatuambia sisi kwamba wananchi wa jimbo la Chalinze hawaridhiki na hali ya ufaulu wa watoto wetu, mazingira bora yapo, "amesema Kunenge na kuongeza

"Tuna changamoto za walimu nimesikia tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunaboresha najisikia fahari, faraja kuwa sehemu ya jamii kuwa sehemu ya jitihada ya kuboresha maisha ya wana Chalinze iwe ya mfano "  amesema Kunenge

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watumishi, madiwani na wananchi kuendelea kumpa ushirikiano mbunge Ridhiwani kwa sababu ameonyesha anawajali kwa vitendo.

"Mbunge huyu ameonyesha anawajali, mara nyingi amekuwa akijitahidi kuonyesha kwa vitendo anawajali, ni mtumishi ambaye anazingatia kutatua kero za wananchi, hizi fedha za madawati angeweza kufanya mambo mengine ya kumjenga yeye binafsi” amesema

Amesisitiza nia yake kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali ni kuhakikisha pale  Chalinze walipofikia sasa wanaboresha zaidi  na kwenda kwa kasi kubwa ili kuleta maendeleo

Awali Ofisa elimu sekondari wa Chalinze, Salama Ndyetabura  ametaja shule zitakazopewa madawati hayo ni Kikaro, Changarikwa ,Pera, Chamakweza ,Moreto, Chalinze, Ubena , Talawanda, Vigwaza ,Rupungwi, Kimange na Kibindu .

Ndyetabura ameongeza kuwa halmashari hiyo kwa kipindi cha mwaka ujao wa fedha wametenga bajeti ya Sh28 milioni kwa ajili kutengeneza madawati yaliyobakia yanayokadiriwa kuwa ni 364.