Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ridhiwani: Kiongozi siyo cheo ni kuonyesha njia

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa kufunga mafunzo elekezi kwa wakuu wa taasisi walioteuliwa hivi karibuni.

Muktasari:

  • Tangu programu Mafunzo Elekezi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali ilipoanzishwa mwaka 2024, zaidi ya Watendaji Wakuu 187 wamepatiwa mafunzo hayo, huku viongozi wapatao 57 wakishiriki katika awamu ya mwaka huu.

Dar es Salaam. Serikali imewataka watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuwa viongozi wa mabadiliko kwa kuonyesha njia kupitia matokeo ya kazi badala ya kutegemea mamlaka ya vyeo walivyo navyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete jana Julai 24, 2026 wakati akifunga Mafunzo Elekezi kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali walioteuliwa yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.

Ridhiwani amesema Serikali inatarajia viongozi hao watakaporejea kwenye taasisi zao wakiwa wamebadilika na tayari kuleta mageuzi yanayoonekana katika utendaji.

“Kiongozi ni kuonyesha njia. Tunategemea kutokea kwenu mtupelekee furaha kwa watumishi wa umma kwa sababu wakiwa na furaha wakitekeleza majukumu yao ndipo serikali inakaa vizuri onyesheni njia ili kupata matokeo badala ya kutumia mamlaka mliyonayo,” amesema Ridhiwani.

Amewataka viongozi hao kwenda kujenga mazingira ya kazi yanayochochea ubunifu, ushirikiano na ustawi wa watumishi ili kuongeza tija katika taasisi pia kujenga uhusiano wa kitendaji wenye afya baina yao na watumishi mnaowasimamia.

Amesema mafunzo hayo hayapaswi kubaki kuwa kumbukumbu ya siku tatu, bali yawe mwanzo wa safari mpya ya kujenga taasisi zenye ufanisi na uwajibikaji.

“Leo hatufungi mafunzo ila tunafungua ukurasa mpya wa utekelezaji wa majukumu yetu. Mafunzo haya yanakuwa na maana endapo maarifa, uzoefu na mbinu zilizofundishwa zitaonekana katika maamuzi na utekelezaji wa majukumu yetu,” amesema.

Ridhiwani amesema viongozi wa taasisi za umma wataendelea kupimwa kwa matokeo wanayoyazalisha, ikiwemo kuondoa urasimu usio wa lazima, kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza tija.

Amewataka kulinda uadilifu wa taasisi wanazoziongoza na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani na Serikali kupitia huduma wanazopata.

“Naomba niwasihi muendelee kulinda uadilifu wa taasisi mnazoziongoza, uaminifu kwa wananchi kwa serikali yao ujengwe pia,” amesema.

Pia, amewataka watendaji hao kutumia muda waliokutana pamoja kujenga mahusiano ya kikazi yatakayorahisisha ushirikiano kati ya taasisi badala ya kila mmoja kufanya kazi kivyake.

“Tengenezeni mahusiano miongoni mwenu kwa sababu yako mengi ya kusaidiana, mengineyo yakiwepo hata yaliyo nje ya maeneo yetu ya kazi,” amesema.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu amesema moja ya mafanikio ya mafunzo hayo ni kuwajenga viongozi wanaofahamiana na kushirikiana zaidi katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Kulikuwa na nafasi nzuri ya kubadilishana mawazo ya kuweza kujuana lakini kuendelea kutengeneza ukaribu wa kufanya kazi pamoja kwa sababu kweli wakuu wa taasisi tunatamani sana tusijuane tu lakini tuwe na ushirikiano,” amesema Mchechu.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi yanayoendelea kufanyika katika taasisi za umma huku akibainisha kuwa mafanikio hayaishii kwenye fedha pekee bali pia yanaonekana katika ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Mchechu amesema taasisi nyingi zimeendelea kuboresha utendaji wake na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka Serikalini huku akieleza kuwa mkutano ujao wa Arusha utatoa nafasi ya kutathmini kwa kina mageuzi hayo na kujifunza kutoka kwa uzoefu wa mataifa mengine.