Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ridhiwani aanza ziara Tabora, azindua miradi ya afya na miundombinu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akizungumza na wananchi baada ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Igunga.

Muktasari:

  • Waziri Ridhiwani Kikwete ameanza ziara ya siku tatu mkoani Tabora kwa kuzindua na kukagua miradi ya afya, daraja na makazi ya watumishi katika wilaya za Igunga na Nzega.

Tabora. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, ameanza ziara ya siku tatu mkoani Tabora kwa kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya za Igunga na Nzega, akisema Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii na miundombinu kwa manufaa ya wananchi.

Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Kining'inila kilichopo kijiji cha Iyogelo, kata ya Kining'inila wilayani Igunga. Mradi huo wenye thamani ya Sh250 milioni unatarajiwa kupunguza adha ya wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Amesema Serikali itaendelea kupeleka miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

"Mradi huu utapunguza adha ya upatikanaji wa huduma za afya. Huu ni mwanzo tu, mazuri mengi yanakuja," amesema Kikwete.

Daraja la Nyandekwa linalojengwa katika Kata ya Nyandekwa, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, likiwa miongoni mwa miradi ya maendeleo iliyokaguliwa wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.

Ujenzi wa kituo hicho ulianza Oktoba 7, 2025 na unatarajiwa kukamilika Julai 30, 2026 ili kuanza kutoa huduma kwa wakazi wa Kining'inila na maeneo jirani.

Diwani wa Kata ya Kining'inila, Amos Weja, alimuomba Waziri Kikwete kuiwezesha kituo hicho kwa gari la wagonjwa ili kurahisisha rufaa za wagonjwa, hususan wajawazito wanaohitaji huduma za dharura.

Mkazi wa Iyogelo, Rozana Marseli, amesema kabla ya mradi huo wananchi walilazimika kutembea kwa saa tano kufuata huduma za afya, hali iliyowaweka katika hatari kutokana na umbali na mazingira ya porini.

"Tulikuwa tunaondoka alfajiri na kurejea nyumbani jioni. Tumeteseka sana, hivyo kituo hiki kitakuwa msaada mkubwa kwetu," amesema.

Wananchi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akihutubia baada ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Igunga.

Naye Bernard Sagija amesema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa kilio cha muda mrefu cha wananchi na utarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Kikwete pia amekagua na kuzindua Daraja la Mawe la Nyandekwa lenye urefu wa mita 25.5 katika Jimbo la Manonga, wilayani Igunga. Daraja hilo limegharimu Sh203.86 milioni na linatarajiwa kukamilika Julai 17, 2026.

Amewataka wananchi na viongozi wa eneo hilo kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni.

Daraja hilo linaunganisha barabara ya Nyandekwa hadi Mwabubele, ambayo ni njia muhimu kwa usafirishaji wa mazao na huduma nyingine za kijamii.

Akiwa wilayani Nzega, Waziri Kikwete pia amezindua nyumba mbili za wakuu wa idara katika Halmashauri ya Mji wa Nzega zilizojengwa kwa gharama ya Sh280.869 milioni, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma.

Ziara ya Waziri Kikwete mkoani Tabora inatarajiwa kuendelea katika wilaya zote saba za mkoa huo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.