RIPOTI MAALUMU: Janga la shahada za ‘mchongo' kwenye vyuo vikuu nchini

Kwa idadi kubwa tu, wanafunzi wanaomaliza na kufaulu masomo ya shahada ya kwanza au ya uzamili ripoti zao za utafiti au tasnifu huandaliwa na kuandikwa na watu wengine wanaojipatia kipato kwa kazi hiyo.

Hiyo ni baada ya uchunguzi uliofanywa na Mwananchi hivi karibuni na kubaini kuwa wanafunzi wengi wa shahada ya kwanza na ile ya uzamili katika vyuo vikuu nchini wanakodi watu binafsi kuwaandikia tasnifu na ripoti za utafiti kwa malipo ya fedha.

Wanachofanya wanafunzi hao ni kuandaa jina au pendekezo la utafiti na pindi linapopitishwa na wasimamizi wao kinachofuata ni kuwakabidhi watu hao shughuli zote zinazofuata.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini pia ongezeko la ‘ofisi’ na watu binafsi waliojiajiri kufanya kazi hiyo ya udanganyifu wa kitaaluma, huku idadi kubwa ya wateja ikiwa ni wanafunzi wa kozi za uzamili ambao wengi wao ni waajiriwa serikalini na kwenye sekta binafsi.

Wataalamu wa masuala ya elimu wanaonya kuwa kuibuka kwa wingi wa watu wanaowasaidia wanafunzi kufanya udanganyifu kunaweza kushusha ubora wa elimu na kuleta athari kubwa katika soko la ajira nchini.

Ingawa hakuna utafiti wa kina uliofanywa kuhusu aina hii ya udanganyifu wa kitaaluma, tatizo hili limekemewa wiki iliyopita na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akiiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuvitangaza vyuo na wasimamizi watakaopitisha mawasilisho ya utafiti bila kuzingatia maadili na ubora.

Pamoja na hatua hiyo, wataalamu wa masuala ya elimu wanavitaka vyuo vikuu viungane na kufanya utafiti wa kina na kutafuta njia za kupambana na hali hiyo.


‘Ofisi’ za tasnifu

Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha ongezeko la ofisi ndogondogo na watu binafsi wanaofanya kazi ya ‘kuzalisha’ tasnifu na ripoti za tafiti kwa malipo ya fedha.

Watu hao wamefungua ofisi zao kuzunguka kampasi za vyuo, wengine wakiajiri mawakala wa kuwatafutia wateja.

Wanafunzi waliozungumza na Mwananchi wanasema mchezo huo ni maisha ya kawaida kwenye baadhi ya vyuo, huku wengine wakisema bila woga kuwa wako tayari kukodi watu wa kuwaandikia tasnifu.

Mkoa wa Dar es Salaam ambao unaongoza kwa kuwa na vyuo vingi vya umma na binafsi ndio kitovu cha biashara hiyo huku mikoa mingine kama Mwanza, Arusha, Morogoro na Dodoma nayo ikitajwa.

Watu wanaofanya kazi hiyo ni baadhi ya wahadhiri walioko kazini na waliostaafu, wanataaluma na wengine wenye vipaji ambao wameamua kuachana na ajira nyingine na kujiunga na kazi hiyo inayowalipa zaidi.

“Umekwishaanda concept note au project title yako? Wengine huniandalia hivyo kabisa na mie hufanya kazi inayobaki. Kwa hiyo nitumie title ya proposal yako iliyokubaliwa na mwalimu wako ili nikupe terms (masharti) za service (huduma),” anasema mwanataaluma wa Morogoro (jina linahifadhiwa) ambaye amejiajiri kwa kuwaandikia wanafunzi tasnifu akimwambia mwandishi wetu aliyekwenda kama mhitaji wa huduma.

Mtu huyo alimwambia mwandishi wetu kuwa amekuwa akijihusisha na biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 10.

“Ninachotaka kukuhakikishia ni kwamba kazi ninayokwenda kukuandalia itapita bila kikwazo. Sijawahi kuwa na kesi ya kukataliwa ripoti ya mtu ambaye nilimwandikia, navijua viwango vinavyotakiwa na nini hasa wasimamizi wanataka,” anasema.

Mwanataaluma mwingine wa jijini Dar es Salaam amekiri kuwa kwa miaka minne sasa amekuwa akiendesha maisha yake kwa kuwaandikia wanafunzi tasnifu na ripoti za utatifi.

Haoni shida yoyote kujihusisha na udanganyifu huo, akisema anafanya shughuli hiyo kuwasaidia wanafunzi kufikia ndoto zao za mafanikio.

Amekwenda mbali zaidi kwa kuiomba Serikali itambue kazi yao na iwaruhusu wanafunzi kutumia huduma zao bila kikwazo.

“Ninachokifanya ni kuwasaidia wanafunzi kufikia ndoto zao. Wananipa research proposals (pendekezo la utafiti) na maelekezo mengine, mimi nafanya kazi iliyobaki. Ninawakusanyia data (taarifa) kwa makubaliano. Mwisho wa siku watalazimika kuisoma kazi yote na kuitetea chuoni, sasa tatizo liko wapi?” anahoji.


Nchi jirani wamo

Uchunguzi huo pia umebaini kuwa baadhi ya raia nchi jirani ni miongoni mwa waliojiajiri nchini kwa kuwaandikia wanafunzi tasnifu hizo.

Wanafunzi wanaonekana kupendelea zaidi waandishi wa nchi jirani kwa madai kuwa wana uwezo mkubwa wa kuandika Kiingereza kizuri na kwamba kazi zao huwa na nafasi kubwa ya kukubalika.

“Yangu iliandaliwa na dada mmoja wa nchi jirani (anaitaja) kwa Sh1.5 milioni, ni nzuri sana! sana! Ongea naye kuhusu yako na utaona mwenyewe,” anasema mwanafunzi aliyemaliza, kutetea na kufaulu vizuri shahada yake ya uzamili katika chuo kimoja cha Dar es Salaam.

Baadhi ya wanaofanya shughuli hii wamebandika matangazo mtandaoni na kwenye ofisi zao zilizo jirani na vyuo vikuu ili kuwapata wanafunzi kwa urahisi zaidi.

Msichana wa miaka 22 ambaye amemaliza hivi karibuni na kufaulu shahada ya kwanza katika Mawasiliano ya Umma anasema anajua wanafunzi wengi aliomaliza nao ambao tasnifu zao zilifanywa na watu waliokodiwa kwa malipo.

“Yangu niliandika mwenyewe kwa sababu sikuwa na pesa ya kumlipa mtu aniandikie, ningekuwa na hela ningempa mtu aniandikie, baadhi wamelipa Sh250,000 wengine hadi Sh400,000,” anasema.

Anasema wanaofanya kazi hiyo wana mawakala. “Wakati mwingine supervisors (wasimamizi) wetu hawajui kinachofanyika, wakati mwingine inategemea na supervisor wako, wengine hawako serious (makini), ukiwapa ripoti wanaonyesha makosa harakaharaka na ukisahihisha hawana muda tena wa kukagua wanakusanya tu.”

Mhariri wa The Chanzo, Khalifa Said anasema udanganyifu wa kitaaluma upo kwa kiwango kikubwa. Anasema anawajua wahitimu wengi ambao walikodi watu kuwaandikia tasnifu na kufaulu masomo yao vizuri.

“Ninachojua ni kwamba suala hili lipo. Ukitaka kufanyiwa utafiti na kuandikiwa ripoti watu wapo,” anasema.

“Tatizo hili ni kubwa kwa post-graduate students (wanafunzi wa masomo ya uzamili), wameajiriwa na wana uwezo wa kumudu gharama za kulipia dissertation (tasnifu) ya kuandikiwa.”

“Binafsi nilifuatwa na mtu ili anifanyie kwa Sh500,000, hiyo ilikuwa mwaka 2016. Nilimkatalia lakini ninge-bargain (bembeleza) angeshuka hata kwa Sh300,000.”

Anasema wanaofanya kazi hiyo ni wanafunzi waliohitimu vyuo vikuu na baadhi ya wahadhiri.

“Supervisor (msimamizi) anakwambia anaweza kukufanyia au anajua mtu anayeweza kukufanyia. Wanafunzi huona ni salama zaidi kumtumia supervisor kuliko mtu wa nje,” anasema.

Mhadhiri katika chuo kimoja Iringa ambaye aliomba kutotajwa jina anasema tatizo la udanganyifu wa kitaaluma lipo na ni kubwa lakini akasema jitihada zozote za kupambana nalo lazima ziendane na masilahi ya wahadhiri.

“Wahadhiri wanalipwa mishahara midogo sana, hawawezi hata kutunza familia zao, kwa hiyo wanafanya kila lililo ndani ya uwezo wao kujaribu kuziba pengo hilo la mishahara isiyotosha.


Tatizo maadili

Kwa mujibu wa Said, ubaya wa suala hilo usiangaliwe tu katika uhalali au kutokuwa halali kwake, bali kwa jicho pana la kuporomoka kwa maadili ya kitaaluma na jinsi ya kuyarudisha.

Anasema jitihada zozote za kupambana na tatizo hilo lazima ziangalie kwanza tatizo la kuporomoka kwa maadili na uadilifu miongoni mwa wanafunzi na wasimamizi na si kuanza kwa kupambana na wanaofanya kazi hiyo.

“Ni tatizo la kimaadili. Ni jinsi gani tunakuza na kusimamia maadili kwa wanafunzi wetu na wasimamizi wao, ndilo lingekuwa jambo la kupewa kipaumbele kwa yeyote anayetaka kupambana na tatizo hilo.

“Lazima tutafute njia za kukuza uwajibikaji wa kimaadili tangu wakati wanafunzi wakipokewa vyuoni. Tatizo ni kwamba watu hawajali chochote kuhusu maadili na miiko ya kitaaaluma. Tumekuwa watu ambao hawaoni hata tofauti kati ya lililo sahihi na lisilo sahihi. Hilo ndilo tatizo.

“Karibu kila tatizo tunaloliona kwenye jamii yetu linatokana na kuporomoka kwa maadili. Hatuwezi kujenga nchi kwa kutumia watu ambao wametumia njia za uongo kujipatia sifa za kitaaluma,” anasema.

Baadhi ya viongozi wa vyuo vikuu waliozungumza na Mwananchi wanakiri kujua uwepo wa tabia hii ambayo wanadai ni ngumu kupambana nayo.

Hata hivyo, baadhi ya vyuo vimechukua hatua kadhaa kudhibiti udanganyifu wa kitaaluma ikiwamo huu wa kuandikiwa tasnifu au kutumia kazi za watu wengine, jambo ambalo limeendelea kustawi na kubaki kuwa tatizo kubwa linalotishia ubora wa elimu nchini.


Msimamo UDSM

“Hilo nimelisikia lakini sina evidence (ushahidi) kwamba wanafunzi wangu wanafanyiwa. Ni kweli wako watu hapa mjini wanaishi kwa kuwaandikia watu, mimi ni associate dean wa School of Education, kwa uzoefu tumewahi kugundua wanafunzi wanaofanyiwa hizo kazi,” anasema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye.

Anasema mifumo ya kukabiliana na tatizo la udanganyifu wa kitaaluma iliyowekwa na UDSM inatoa jibu la kwa nini watu wengine wamekuwa wakikwepa kusoma chuoni hapo katika ngazi ya shahada ya kwanza na uzamili.

Anasema chuo chake kimeweka mfumo thabiti wa kugundua wanafunzi wanaoandikiwa kazi au wanaotumia kazi za watu wengine zilizofanywa miaka ya nyuma.

“Uongozi wa chuo chetu unafanya kila liwezekanalo kuhakikisha quality assurance (uhakika wa ubora). Hapa UDSM hata mwanataaluma akiletwa tunamwambia alete machapisho yaliyomfanya awe profesa, that’s what we normally do (hicho ndicho tunachofanya) kuhakikisha quality (ubora) yetu haishuki. Hatutaki mtu atuharibie sifa tuliyoijenga kwa miaka 61,” anasema.


Saut: Tunadhibiti

Mkuu wa Kitengo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Mwanza, Dk Peter Mataba anasema uongozi wa chuo hicho unafahamu uwepo wa udanganyifu kwa baadhi ya wanafunzi wakati wa utafiti na umeweka mifumo imara kubaini na kudhibiti vitendo hivyo.

“Kuna watu wanafanya kazi ya kuwafanyia tafiti wanafunzi wa elimu ya juu; wengine hadi wanajitangaza. Sisi Saut tumeweka mifumo kubaini na kudhibiti udanganyifu huu,” anasema Dk Mataba.

Anasema mifumo hiyo ambayo ni ya lazima kwa vitivo, idara na wahadhiri wote wa Saut inalenga kudhibiti na kulinda ubora wa elimu.

“Tunasisitiza wasimamizi wawili akiwamo mmoja wa nje kuondoa uwezekano wa kuwapo makubaliano ya kufanya udanganyifu. Hata kama mwanafunzi atashirikiana na msimamizi wa ndani kwa sababu wanafahamiana, hawezi kufanya hivyo kwa msimamizi wa nje kwa sababu hawafahamiani,” anasema.

Ufuatiliaji wa karibu na vikao vya mara kwa mara kati ya wanafunzi na wasimamizi wao ni mbinu nyingine inayotumiwa na Chuo cha Saut kubaini iwapo tafiti zinafanyika kwa mujibu wa maelekezo, mbinu na muda sahihi.

Dk Mataba anasema wanafunzi wanaofanya udanganyifu pia hubainika wakati wa vikao vya kutetea tasnifu zao… “Mtu aliyefanya kazi yake kwa ukamilifu na uhakika anakuwa na uelewa mpana na wa kina wa topic na hoja zote; aliyefanya udanganyifu siyo tu hukosa uelewa mpana, bali pia hubabaika wakati wa kutetea andiko lake mbele ya jopo,” anasema Dk Mataba.

Anasema Saut inatumia teknolojia kubaini tafiti zilizonakiliwa… “Tunatumia Plagiarism test technology (teknolojia ya kubaini wizi wa kazi za watu) kubaini tasnifu zilizonakiliwa. Mtafiti ni lazima asome, apitie na kunukuu machapisho na tafiti zingine, lakini ni jambo lisilokubalika mtafiti anapobainika kunakili au kunukuu tafiti zilizotangulia kwa asilimia 50.”

Pamoja na kutumia teknolojia kubanini udanganyifu, vyuo vikuu pia vimetakiwa kutotegemea sana teknolojia hizo kwa sababu wanaofanya hivyo wanatumia mbinu za juu zaidi kufanikisha udanganyifu wao.

Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo ya Uzamili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Donatha Tibuhwa anasema hata ukiwa na teknolojia inaweza isisaidie pale mwanafunzi anapoamua kutumia kazi ya mtu iliyofanywa miaka mingi iliyopita na ambayo haikuingizwa kwenye mitandao.

Anasema tatizo la udanganyifu wa kitaaluma si jambo geni duniani, “kimsingi ni tatizo la dunia. Imefikia wengine wanajitangaza kabisa kwenye mitandao. Sisi tunafanya kila lililo katika uwezo wetu kuhakikisha haliingii katika chuo chetu,” anasema.

Anasema UDSM ambayo kwa mwaka huzalisha wanafuzi takriban 8,000 wa shahada ya kwanza na wengine kati ya 900 na 1,000 wa shahada ya uzamili, imekuwa ikifanya mafunzo na semina mbalimbali kwa wahadhiri wanaoajiriwa na chuo hicho na wanafunzi wapya kuwaandaa kulinda tunu zake.

Kama vilivyo vyuo vingine, Profesa Tibuhwa anasema UDSM pia inatumia teknolojia mahsusi ya kupima umiliki wa tasnifu kwa wanafunzi.

Anaomba hatua kali zichukuliwe dhidi ya wale wanaojitangaza hadharani na mitandaoni kufanya kazi ya kuwasaidia wanafunzi kufanya udanganyifu.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya elimu, John Kalage naye anasema wamewahi kusikia taarifa za wanafunzi kufanya udanganyifu.

“Tumewahi kusikia lakini hatujawahi kufanya utafiti, hatuna ushahidi,” anasema.

Hata hivyo, anaeleza kuwepo wanafunzi ambao uwezo wao wa kitaaluma unaosomeka kwenye vyeti hauendani na wanachoonyesha wakiwa kazini. “Tunahitaji kufanyia utafiti,” alisema.

“Unaona mtoto anafanya mtihani wa kidato cha pili hajui kusoma wala kuandika, kwa hiyo ukichambua hiyo hali unapata majibu.

“Kijana anayehitimu shahada ya kwanza hafanani na uwezo wa kitaaluma unaoonekana kwenye cheti chake. Kama ni daktari anaweza kuwaweka wagonjwa kwenye hatari kubwa na kama ni mhandisi basi inaweza kuwa hasara kubwa kwa uchumi,” anasema.

Kalage anashauri kubadilishwa kwa mfumo wa tathmini ya wahitimu ili usitoe nafasi kwa mtu aliyefanya udanganyifu kupata alama za juu katika masomo.

“Tuangalie namna ya kuwatathmini wahitimu wetu. Kilichotokea LST (Shule ya Uanasheria kwa Vitendo) ni kwamba products waliokuwa wanazalishwa na vyuo kutoka chini walikuwa dhaifu sana. Watu wanadanganya kuanzia chini hadi kazini,” anasema akisisitiza kuwa kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanathamini zaidi cheti badala ya elimu.

Kuhusu hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzan Ndomba-Doran anasema, “kuna utafifi tunaofanya kwenye eneo hili na ripoti ikitoka tutakutaarifu.”


TCU yatia neno

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Charles Kihampa anasema si rahisi kwa tume yake kuthibitisha au kutothibitisha uwepo wa udanganyifu wa kitaaluma na kwa kiwango gani bila kuwa na ushahidi.

Sheria inayounda TCU imeipa majukumu kadhaa likiwamo la kusimamia na kudhibiti uendeshaji wa vyuo vikuu pamoja na kudhibiti ubora wa viwango vya elimu inayotolewa na vyuo hivyo.

“Nachelea kusema tatizo lipo lakini sisi kama wadhibiti ubora tumeweka minimum standards (viwango vya chini) to ensure ownership (kuhakikisha umiliki) ya kazi ya mwanafunzi. Kwa hiyo, mwanafunzi lazima afanye presentation (uwasilishaji) ya tasnifu aliyofanya mbele ya jopo la wahadhiri, kama kazi si yake utagundua tu. Vile vigezo tulivyoweka kwa wanafunzi wa PhD na Master’s ni kwa jili ya kuhakikisha ownership,” anasema.

Anasisitiza kuwa TCU imeweka viwango vya kuhakikisha mwanafunzi ndiye mmiliki halisi wa kazi tangu katika hatua ya kuandika pendekezo la utafiti, kuitetea mbele ya jopo na takwa la kufanya machapisho.

“Uwezekano wa watu kudanganya upo ndio maana TCU tupo lakini pia miongozo ya kuhakikisha umiliki ipo,” anasema.

Anasema ni vyema watu wakafahamu kuwa kazi ya TCU si kuvisimamia vyuo vikuu kama polisi, bali kuvisaidia vijiendeshe kwa mujibu wa sheria na kuruhusu ubunifu miongoni mwa vyuo.