Ripoti yalaumu Uingereza kumuondoa Gaddaffi

Aliyekuwa kiongozi nchini Libya, Kanali Muammar Gaddafi wakati wa uhai wake

Muktasari:

Kamati hiyo ya Mambo ya Nje imesema Uingereza iliongeza chumvi ilipokuwa inaeleza hatari ambazo zingewakumba raia baada ya serikali ya Gaddafi kuanza kukabiliana na maasi.

Ripoti ya kamati ya bunge nchini Uingereza imekosoa hatua ya Uingereza na Ufaransa kuingilia kati na kusaidia kuondolewa mamlakani kwa Kanali Muammar Gaddafi nchini Libya mwaka 2011.

Kamati hiyo ya Mambo ya Nje imesema Uingereza iliongeza chumvi ilipokuwa inaeleza hatari ambazo zingewakumba raia baada ya serikali ya Gaddafi kuanza kukabiliana na maasi.

Mpango wa kuingia kati kusaidia mwishowe ulitumiwa kama fursa ya kubadilisha utawala, ripoti hiyo inasema.

Ripoti hiyo inamtuhumu aliyekuwa waziri mkuu David Cameron kwa kukosa kuandaa mkakati mahsusi kuhusu Libya.

Wabunge hao wanasema hilo lilisababisha kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, mzozo wa wahamiaji, ukiukwaji wa haki za kibinadamu na kukua kwa kundi la wapiganaji wa Kiislamu wanaojiita Islamic State Afrika kaskazini.

Msemaji wa serikali ya Uingereza ametetea serikali na kusema muungano wa mataifa ya Kiarabu, Arab League, pamoja na Umoja wa Mataifa, wote waliunga mkono hatua hiyo ya kijeshi.

Gaddafi aliuawa na waasi 20 Oktoba, 2011.