RPC: Anayedaiwa kubakwa, kulawitiwa na vijana wa ‘afande’ ni kama anajiuza
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limesema limekamilisha uchunguzi wa kesi inayowakabili vijana wanaodaiwa kutumwa na ‘afande’. Limesema vijana hao wamekiri hawakutumwa na binti anayedaiwa kutendewa tukio hilo anaonekana alikuwa anajiuza.
Mbeya. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya amesema jalada la kesi ya vijana watano wanaotuhumiwa kutekeleza tukio la ubakaji na ulawiti wa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam limekamilika.
Vijana hao wanaodaiwa kutumwa na afande, wanne kati ya sita wameshakamatwa ambao walipanga na kutekeleza uhalifu huo. Tukio hilo liliibua mijadala mikali maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandaoni.
Ukamataji huo umewagusa pia watu wengine wanane, kati yao wakiwemo wanne waliokamatwa kwa kukiuka sheria na kusambaza picha mjongeo (video) za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, zilizoonyesha tukio hilo la ukatili.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, iliyotolewa Agosti 9, 2024 na Msemaji wake, David Misime ilisema video hiyo ilianza kusambaa Agosti 2, 2024 kupitia mitandao ya kijamii ikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti msichana mmoja wakidai kuagizwa na afande.
Amewataja waliokamatwa kwa kosa la kumlawiti na kumbaka binti huyo ni Clinton Damas jina maarufu Nyundo, Praygod Mushi, Amini Lema na Nikson Jakson.
Misime alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika mikoa ya Dodoma na Pwani, huku jeshi hilo likiendelea kuwasaka watuhumiwa wawili ambao hawajapatikana hadi sasa.
Jana Jumapili, Agosti 18, 2024, RPC wa Dodoma, Theopista akizungumza na Mwananchi lililotaka kujua nini kinaendelea juu ya watuhumiwa hao, alisema katika uchunguzi Jeshi la Polisi lilibaini vijana hao waliotuhumiwa kwa madai ya kutumwa, walikiri kutoagizwa na askari kama ilivyoelezwa.
"Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza 'kahaba'."
"Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo" alisema Kamanda huyo.
Endelea kufuatilia Mwananchi.