RPC Songwe awasaka waliowapiga viajana watatu mkutano wa Chadema

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, ACP Theopista Mallya.
Tunduma. Kamanda wa Polisi mkoa Songwe, ACP Theopista Mallya amesema Jeshi hilo linawasaka watu waliowajeruhi vijana watatu wakiwatuhumu kumwaga pilipili katika mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika jana Jumamosi Oktoba 21, 2023 kwenye Uwanja wa shule ya sekondari Mwalimu Nyerere Mjini Tunduma mkoani hapa.
Akizungumza leo Jumapili Oktoba 22, 2023 kamanda huyo amesema Polisi waliwaokoa vijana watatu ambao walikuwa na umri wa miaka 15, mwingine 16 na mwingine 19 ambao baada ya kuokolewa toka mikononi mwa watu wanaojiita walinzi wa Chadema walipelekwa kituo cha Polisi na walipatiwa fomu ya PF3 kwa ajili ya matibabu.
"Baada ya kupatiwa PF3 walikwenda kutibiwa hospitali na kisha Kufungua kesi ya shambulio kama ulivyoona ‘clip’ inayozunguka mitandaoni" amesema Mallya.
Amesema kufuatia shambulio hilo hakuna mtu aliyekamatwa, lakini wale wote waliohusika watasakwa hadi wakamatwe kwani wameonekana na kufikishwa mahakamani ambako watatoa ushahidi wao na vielelezo walivyoviona.
Tukio la vijana hao kupigwa lilitokea jana kwenye, Mkutano wa Chama hicho kufuatia madai kumwaga pilipili kwa vijana hao kwenye eneo la jukwaa kuu hali hiyo ilawalazimu Polisi kuingilia kati kuwaokoa vijana hao kwa kupiga mabomu mawili ya machozi angani.