Rufaa DC Odunga kupinga kutoa Sh7 milioni matunzo ya mwanaye kusikilizwa kwa maandishi

Muktasari:

Mahakama ya Wilaya ya Ilala imetoa siku 14 kwa Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga kuwasilisha hoja za rufaa yake kwa maandishi.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Ilala imetoa siku 14 kwa Mkuu wa wilaya ya Chemba, Simon Odunga kuwasilisha hoja za rufaa yake kwa maandishi.

Odunga alikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Ukonga. Katika hukumu hiyo, Odunga alitakiwa kutoa Sh7 milioni kama nusu ya gharama za matunzo aliyotumia mkewe, Medelina Mbuwuli kumsomesha mtoto wao kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

Odunga alifungua kesi kumtaliki mkewe lakini mahakama ililikataa ombi hilo, badala yake ikamtaka alipe kiasi hicho cha fedha.

Leo Alhamisi Desemba 12, 2019 hakimu Mkazi wa Mahakama ya Ilala,  Glory Nkwera amesema kesi hiyo itaendeshwa kwa maandishi baada ya Medilina kuomba iwe hivyo kwa kuwa hana wakili.

Awali, wakili wa mleta maombi,  Bededict Pius alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajali ya kuanza kusikilizwa na kuomba mahakama kutoa mwongozo.

Hakimu Nkwera alimuuliza  Medilina  kama ana wakili, na mke huyo wa Odunga kujibu kuwa hana na kuomba kesi hiyo kuendeshwa kwa maandishi.

Hakimu Nkwera ameutaka upande wa waleta rufani kuwasilisha hoja za rufaa hiyo kwa maandishi Desemba 27, 2019 na  Medelina kuwasilisha majibu Januari 10, 2020.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 17, 2020.