Rufaa kesi ya Gekul yapigwa kalenda

Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Pauline Gekul.

Muktasari:

  • Hukumu ya rufaa ya kesi ya jinai ya shambulio la mwili inayomkabili mbunge wa Babati mjini Mkoani Manyara na aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul iliyokuwa isomwe leo jumatatu Machi 18 mwaka 2024 imeahirishwa hadi Machi 21.

Babati. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, imeahirisha rufaa ya jinai iliyokatwa na Hashim Ally dhidi ya Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul baada ya mjibu rufaa huyo kutopewa wito wa kuitwa mahakamani.

Leo Jumatatu Machi 18,2024 Mahakama hiyo ilipanga kusikiliza rufaa hiyo namba 577/2024, mbele ya Jaji Devotha Kamuzora, lakini kutokana na sababu  zilizo nje ya wadaawa (mrufani na mrufaniwa),  shauri hilo limeahirishwa hadi Machi 21,2024.

Wakili wa mrufani, Peter Madeleka amesema mahakama haijapeleka hati za wito wala nyaraka za rufaa kwa mjibu rufani.

Katika rufaa hiyo, Ally anapinga maamuzi yaliyofanywa na Mahakama ya Wilaya ya Babati Desemba 27, 2023 ya kuiondoa kesi hiyo mahakamani baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Leo Pauline hukuweza kufika mahakamani ambapo Wakili Ephraim Kisanga anayemwakilisha, ameeleza kuwa siyo mteja wao wala wao(mawakili) hawakuwa wamepokea nyaraka zozote za rufaa na badala yake wamesikia taarifa za rufaa hiyo kupitia vyombo  vya habari.

Gekul alidaiwa kumshambulia na kumdhuru Ally Novemba 11, 2023 kinyume cha kifungu cha 41 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya 2022.