DPP afuta kesi dhidi ya Gekul

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul.

Muktasari:

  • Kesi ya unyanyasaji iliyokuwa ikimkabili mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul imetajwa leo kwa mara ya kwanza na  imefutwa kwa maelekezo ya DPP.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Babati imeifutilia mbali kesi ya ukatili iliiyokuwa ikimkabili mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul kuhusiana na tuhuma za unyanyasaji dhidi ya mfanyakazi wake, Hasim Ally.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Babati, Victor Kimario ameieleza Mwananchi Digital kuwa kesi hiyo imetajwa  leo Jumatano Desemba 27, 2023 mbele yake na ameifuta baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea nayo.

“DPP amewasilisha taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi)”, amesema Hakimu Kimario na kufafanua kuwa, hakuna wakili wa Serikali aliyefika mahakamani leo wakati kesi hiyo ilipotajwa na taarifa hiyo wamewasilisha masjala.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Hashimu kupitia kwa wakili Peter Madeleka chini ya kifungu cha 128(2) na (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Wakili Madeleka alilieleza Mwananchi kuwa kifungu hicho kinaruhusu mtu binafsi kufungua kesi ya jinai bila kupitia kwa DPP.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya malalamiko ya kesi hiyo, Gekul alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la shambulio na kusababisha madhara kwa mwili chini ya kifungu cha 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marekebisho ya mwaka 2022.

Alikuwa anadaiwa kuwa yeye na watu wengine ambao hawako katika malalamiko hayo, Novemba 11, 2023, mjini Babati, mkoani Manyara walimuita Hashim na kumuweka kizuizini, huku wakimtishia kwa silaha ya moto, walimvua nguo na  kumshambulia kwa kumlazimisha kukalia chupa ya soda ili iingie katika njia yake ya haja kubwa.

DPP amewasilisha taarifa hiyo ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo chini ya kifungu cha 91(1) cha CPA, kinachompa mamlaka ya kufuta kesi yoyote ya jinai katika hatua yoyote kabla ya hukumu ya Mahakama na bila kulazimika kutoa sababu za uamuzi huo.