Rufaa ya Sabaya, wenzake yakwama

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya akizungumza na Mawakili wake, Mosses Mahuna na Fauzia Mustapa, nje ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha leo Novemba 15,2023. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Mahakama ya Rufaa Tanzania imeahirisha kusoma hukumu ya rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili baada ya wajibu rufaa wenzake wawili kushindwa kufika mahakamani.

Arusha. Mahakama ya Rufaa Tanzania imeahirisha kusoma hukumu ya rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili baada ya wajibu rufaa wenzake wawili kushindwa kufika mahakamani.

 Katika rufaa hiyo Jamhuri inapinga hukumu ya Mei 8, 2022, iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliyomuachia huru Sabaya na wenzake Sylvester Nyegu na Daniel Mbura.

Leo Jumatano Novemba 15, 2023 mahakamani hapo mjibu rufaa mmoja (Sabaya) pekee ndiye aliyekuwepo mahakamani, huku wajibu rufaa wenzake wawili wakidaiwa kuwa nje ya Arusha na wako njiani kurudi hivyo mahakama kuamua kuahirisha hadi Novemba  17,2023.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Abeesiza Kaleyegeya, alisema kutokana na wajibu rufaa wawili kutokuwepo hukumu hiyo inaahirishwa hadi Novemba 17, 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, Wakili Mosses Mahuna, anayemwakilisha Sabaya, amesema ni takwa la kisheria wajibu rufaa lazima wawepo siku ya hukumu.

Rufaa hiyo namba 231/2022 ilisikilizwa na jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Jacobs Mwambegele, Ignas Kitusi na Leila Mgonya.

Wakati mawakili wa mleta rufaa wakisema kwenye kesi ya msingi walithibitisha mashitaka yote bila kuacha shaka, upande wa wajibu rufaa walisema kwamba hawakufanya hivyo, huku wakidai kuwa walishindwa kueleza hata eneo lilipo duka.

Wakati hati ya mashtaka ikisema duka lipo mtaa wa Bondeni baadhi ya mashahidi wakidai duka hilo lipo Soko Kuu.

Mleta rufaa (DPP), anawakilishwa na jopo la mawakili wanne wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Chivanenda Luwongo, ambaye aliomba kufanya marekebisho ya hoja za rufaa kutoka saba hadi kufikia tatu baada ya kuunganisha sababu zingine huku nyingine wakiondoa.

Akiwasilisha sababu za rufaa mahakani hapo Novemba 1, 2023 Wakili huyo alitaja sababu ya kwanza kuwa ni kuwa Mahakama ya Rufaa ya kwanza ilikosea kwa kusema kesi yao haina mashiko kwa sababu shahidi namba mbili hakuulizwa maswali na wajibu rufaa namba mbili na tatu na kufuta ushahidi wao wote na akawaachia huru.

Sababu nyingine ni mahakama hiyo kusema usikilizwaji wa awali wa kesi ulikosewa kwa sababu wajibu rufaa wawili (Nyegu na Mbura), kuwa kuna vitu hawakusomewa wakati waliandika kwa maandishi kuwa wametimiza.

Alitaja sababu ya tatu kuwa ni Jamhuri haikuweza kuthibitisha kesi yao pasipo kuacha shaka,jambo ambalo alisema kesi hiyo ilitibitishwa pasipo kuacha shaka yoyote ambapo upande huo wa jamhuri walirejea ushahidi na vielelezo mbalimbali vilivyowasilishwa kwenye kesi ya msingi.

Aidha wakili huyo alieleza mahakama kuwa ushahidi wa shahidi wa pili wa jamhuri siyo ushahidi pekee uliowatia hatiani wajibu rufani hao na kuwa ushahidi wa mashahidi wengine na vielelezo viliwatia hatiani washitakiwa hao.

Wakili wa wajibu rufaa Mahuna,akijibu hoja hizo alirejea ushahidi uliotolewa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha akieleza ni msimamo wao kuwa hukumu ya rufaa ya kwanza ilikuwa sahihi na haikuwa na mapungufu yoyote.

Mahuna aliendelea kusisitiza msimamo wa kuwa utaratibu wa hoja za awali haukufuatwa kama ambavyo mahakama ya kwanza ya rufaa imeona na inatokana na upande wa jamhuri kushindwa kufanyia marekebisho hati ya mashitaka huku akinukuu mashauri mbalimbali.

Alieleza kuwa ni uelewa wao kwamba haki yakusikilizwa ni moja ya haki ya msingi na kitendo cha mjibu rufaa wa pili na tatu kutopewa nafasi ya kumuuliza maswali ya dodoso kiliwanyima haki ya kusikilizwa na kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haisemi kiwango cha haki ya kusikilizwa.

Hukumu anayoipinga DPP ilitolewa Mei 6, 2022 na Jaji Sedekia Kisanya wa mahakama Kuu Kanda ya Musoma ambaye alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona kulikuwa na mkanganyiko kwenye mwenendo wa usikilizwaji wa shauri kwenye mahakama ya haki mkazi Arusha.


Alieleza kuwa kulikuwa na  kutofautiana kwa mashahidi na kuufanya ushahidi kuwa batili na Mrufani namba mbili  Nyegu na  tatu Mbura hawakupewa haki ya kumhoji shahidi namba mbili wa Jamhuri hivyo kunawanyima haki yao msingi.

Awali Oktoba 15, 2021 Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, aliwahukumu Sabaya na wenzake wawili kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Akitoa hukumu hiyo,Hakimu Amworo alisema ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake ambapo katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa na mashahidi 11 na vielelezo vinane.

Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka 2021 baada ya kukamatwa Meo 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.